Waziri Ummy:Kero ya watu wengi hapa ni gharama za matibabu, tumepokea maoni yenu

NA ENGLIBERT KAYOMBO

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuja na mwongozo wa gharama za kumuona Daktari katika Vituo vya kutolea huduma za Afya vya Umma nchini ambao unatarajiwa kuanza kutumika kuanzia mwezi Februari, 2023.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 27, 2022na Waziri wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, kuona hali ya utoaji huduma za afya pamoja na kusikiliza kero, ushauri na maoni ya wananchi juu ya upatikanaji wa huduma za afya nchini.

“Kero ya watu wengi hapa ni gharama za matibabu, tumepokea maoni ya wananchi, Hospitali zetu wamejiwekea gharama bila hata kupewa mwongozo, Sasa hivi Wizara inakamilisha Mwongozo wa uchangiaji gharama za matibabu na utaanza kutumika mwezi Februari 2023,”ameeleza Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inaelekeza wananchi kuchangia gharama za matibabu hivyo kupitia mwongozo huo utatoa mchanganuo wa gharama za kumuona daktari kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo Vya Afya, Hospitali ya Rufaa, Wilaya, Mkoa, Kanda, Maalum na Taifa.
Waziri Ummy amesema hapo awali hakukuwa na mwongozo unaoainisha gharama husika za kumuona daktari hivyo kupelea vituo vingi vya kutoa huduma za afya kuwa na gharama tofauti tofauti zisizoendana hivyo kuleta kero zaidi kwa wananchi.

Waziri Ummy amewataka watoa huduma za afya nchini kuendelea kuboresha huduma wanazotoa ili kutimiza azma ya Serikali ya ubora wa Huduma za Afya nchini kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni na Miongozo inayotolewa na Serikali.

Amesema kuwa huduma za Uzazi, Mama na Mtoto zitaendelea kutolewa bure katika Kliniki za ‘RCH’ na kuwataka watoa huduma kuzingatia maelekezo ya Serikali na kutowatoza wananchi gharama kwa ajili ya huduma hizo.
Katika Hatua nyingine Waziri Ummy ametoa rai kwa wananchi kujiunga na Skimu mbalimbali za Bima ya Afya wakiwa na Afya njema ili kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.

“Matibabu sasa hivi ni gharama, ugonjwa ukija haukwambii nenda kakate Bima ya Afya kesho utaumwa, unaumwa tuu ghafla, tutatoa mwongozo wa gharama za kuchangia gharama za matibabu, lakini ni vyema tukawa na Bima ya Afya,"amesema.
Amesema kuwa, Serikali itaendelea kuweka utaratibu wa kutoa Bima ya Afya baada ya miezi mitatu toka kujiunga ili kudhibiti watu wenye nia ya kutaka kujiunga na Bima ya Afya mara baada ya kuumwa kwa kuwa kufanya hivyo kuna hatarisha uhai wa Mfuko wa Taifa wa Bima na Afya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news