NA MWANDISHI WETU
KATBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara kukutana kila robo mwaka kufanya tathmini ya pamoja ya utekelezaji wa malengo.

"Kikao hiki kimetuleta pamoja Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ambao ni watekelezaji wakuu wa miongozo, Sera na Mipango tunayojiwekea ili kufikia malengo yakiwemo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa na Ilani ya CCM,"amesema Dkt. Francis Michael.

Amezitaka Taasisi pia kushirikisha wadau wakati wa kuandaa mipango ili kujua mahitaji halisi katika Sekta. Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kuwa na mipango sahihi ya kutekeleza katika mwaka.
Katibu Mkuu Michael amepongeza Taasisi kwa kuendelea kutekeleza majukumu kwa ubunifu na kuwataka kuongeza kasi za kuja na mbinu za kibunifu zaidi ili kufikia malengo mapana ya kitaifa.
Katika hatua nyingine Dkt. Michael amewaagiza Taasisi kutangaza kazi kubwa zinazofanyika katika maeneo yao ya kazi kwani wananchi wana ari kubwa ya kusikia mafanikio hayo na si kujibu malalamiko tu.
"Fanyeni kazi na vyombo vya habari na tukifanya kitu kizuri tutangaze na kama kiongozi huwezi mwambie afisa habari aseme," ameeleza Dkt. Michael
Kwa upande wake Abdul-Razaq Badru Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ameipongeza Wizara kwa kuja na mpango huo ambao amesema utasaidia katika kubadilishana uzoefu kutatua changamoto kwa pamoja na kupanga mikakati kwa pamoja kujenga timu ili kwa pamoja hatimae kufikia malengo mapana ya sekta.