Wizara ya Mambo ya Nje yaomboleza kifo cha Balozi Celestine Mushy

NA DIRAMAKINI

UONGOZI wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umeeleza kusikitishwa na kifo cha Balozi wa Tanzania nchini Austria na Mwakilishi wa Kudumu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Vienna, Mhe. Celestine J. Mushy aliyefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Mkata, Handeni mkoani Tanga tarehe 13 Desemba, 2022.

Balozi Mushy amefariki dunia baada ya gari aliyokuwa akisafiria kutoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Kilimanjaro kugongana na lori la mizigo na hatimaye kuungua moto na yeye akiwa ndani yake.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 16, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Balozi Mushy atakumbukwa kwa umahiri wake mkubwa katika masuala ya kidiplomasia.

"Wakati wa uhai wake ameitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nafasi mbalimbali zikiwemo Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kaimu Katibu Binafsi wa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne na Katibu Tawala Msaidizi wa Masuala ya Uchumi, Sektetariet ya Mkoa wa Mtwara.

"Wizara kwa kushirikiana na familia ya Marehemu Balozi Mushy inaendelea na mipango ya maandalizi ya mazishi na itakapokamilika wananchi watajulishwa.Wizara inatoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa wa Marehemu kwa kuondokewa na mpendwa wao.Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu Balozi Celestine Mushy mahali pema peponi, Amina,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news