YALIYOSISIMUA 2022: Asilimia 10 ya Mikopo kutoka Halmashauri

NA DIRAMAKINI

SERIKALI imeagiza kufanyika tathmini ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu ili kubaini kiasi kilichorejeshwa na kuwakopesha wahitaji wengine nchini.

Kauli ya Serikali imetolewa hivi karibuni na Mheshimiwa Dkt.Festo Dugange, Naibu Waziri (Afya) Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) alipofanya ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma ambapo aliongea na watumishi wa halmashauri na kutoa maelekezo.

“Fedha zote za mikopo ya asilimia 10 zilizokopeshwa tangu tumeanza mwaka 2018 katika Halmashauri ya Chamwino zijulikane ilikopesha kiasi gani na kiasi gani kimerejeshwa mpaka sasa na kiasi gani hakijarejeshwa, zifanyiwe tathmini ili kujua fedha zinazokopeshwa na zinazorejeshwa,”alisema Dkt.Dugange.

Pia Dkt.Dugange alitaka kuwekwa utaratibu maalum kwa kutumia mfumo uliopo wa mikopo ya asilimia 10 ili kufuatilia kwa ukaribu vikundi vyote viweze kurejesha mikopo kwa wakati na kuwapa fursa wahitaji wengine, lengo likiwa ni kuwakwamua vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kiuchumi katika halmashauri hiyo.

Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2018 iliweka masharti kwa halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu

Aidha, kufuatia marekebisho hayo, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ilitunga kanuni zinazoainisha masharti ya utoaji na usimamizi wa mikopo inayotolewa na halmashauri kwa vikundi hivyo.

Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu zilitangazwa katika Tangazo la Serikali Na.286 la Aprili 5, 2019.

Serikali ilifikia hatua hiyo, ili kuyakwamua makundi hayo kiuchumi, lakini pia kuifanya mikopo hiyo kuwa endelevu ambapo tayari imekwishatengenezewa mifumo mbalimbali ikiwemo ya namna ya utoaji na ufuatiliaji.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, halmashauri ina wajibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato yanayotoka katika vyanzo vyake vya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili.

Aidha, halmashauri itakuwa na wajibu wa kugawa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo kwa kuzingatia mgawanyo wa asilimia 40 kwa ajili ya vikundi vya wanawake.

Asilimia 40 kwa ajili ya vikundi vya vijana na asilimia 20 kwa ajili ya vikundi vya watu wenye ulemavu huku ikielekezwa kuwa, mikopo itakayotolewa na halmashauri chini ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na watu Wenye Ulemavu haitakuwa na riba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news