Yanga SC haikamatiki kileleni mwa Ligi

NA DIRAMAKINI

YOUNG Africans SC unaweza kukiri wazi kuwa, kwa sasa haikamatiki katika kutetea taji la Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, kwani wapo kileleni kwa alama 41 baada ya mechi 16.

Wanajangwani hao ambao ndiyo wanajipa raha kileleni mwa ligi hiyo yenye timu 16, kwao Polisi Tanzania FC wanaugulia maumivu wakiwa nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi hiyo.

Mabingwa hao watetezi wameendelea kujiweka katika nafasi nzuri baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Polisi Tanzania FC.

Ni kupitia mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambao umepigwa leo Desemba 17, 2022 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga SC yamefungwa na Jesus Moloko dakika ya 47, Fiston Kalala Mayele dakika ya 77 na Clement Mzize dakika ya 86.

Katika hatua nyingine,Singida Big Stars kutoka mkoani Singida imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Ni kupitia mtanange wa nguvu ambao umepigw akatika Uwanja wa Sokoine uliopo jijini Mbeya.Mabao ya Singida Big Stars yamefungwa na Bruno Gomes dakika ya tano na Meddie Kagere dakika ya 57, wakati la Tanzania Prisons limefungwa na Jumanne Elfadhil kwa penalti dakika ya 79.

Nayo Ihefu FC imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Mtanage huo wa nguvu umepigwa katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Ihefu FC imepewa raha kupitia mabao yaliyofungwa na Obrey Chirwa dakika ya 85 na Michael Aidan aliyejifunga dakika ya 90.

Aidha,Kagera Sugar ambao walikuwa wenyeji wamelazimishwa sare ya 2-2 na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ni kupitia mtanange ambao umepigwa katika Uwanja wa Kaitaba Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Yussuf Mhilu dakika ya 12 na Meshack Abraham dakika ya 62 ndio waliiwezesha Kagera Sugar kupata mabao hayo, huku Azam FC yamefungwa na Iddi Suleiman dakika ya 68 na Idris Mbombo dakika ya 87.

Kupitia ligi hiyo inayoundwa na timu 16, timu tano ambazo zipo katika nafasi ya juu zaidi ni Yanga SC ambao wapo nafasi ya kwanza kwa alama 41 baada ya mechi 16.

Nafasi ya pili inashikiliwa na Azam FC ikiwa na alama 36 baada ya mechi 16 huku Simba SC ya jijini Dar es Salaam ikishika nafasi ya tatu kwa alama 34 baada ya mechi 15.

Wakati huo huo, nafasi ya nne inashikiliwa na Singida Big Stars FC ambao wana alama 30 baada ya michezo 16 huku nafasi ya tano ikishikiliwa na Mtibwa Sugar FC baada ya mechi 16 ikiwa na alama 23.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news