Algeria yajivunia uhusiano na Iran

ALGIERS-Ebrahim Boughali, Spika wa Bunge la Algeria amesema, wanajivunia mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja mbalimbali na wanataka kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Ameyabainisha hayo Januari 29, 2023 katika mazungumzo na Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyofanyika kati ya maspika wa mabunge ya nchi mbili pembeni ya mkutano wa 17 wa Mabunge ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) nchini Algeria.

Spika Qalibaf na ujumbe aliofuatana nao wapo nchini Algeria kushiriki mkutano wa mabunge ya nchi wanachama wa OIC.

Pia Spika Boghali ameeleza kuwa,suala la kuipigania Palestina ni suala kuu na muhimu na akaongeza kuwa, Algeria inafanya juhudi ili nchi ya Palestina iweze kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Spika wa Bunge la Algeria ameeleza kwamba, hujuma zote dhidi ya Uislamu na kuchomwa moto Qur'ani hivi karibuni vinaonyesha kuwa Uislamu ndio ukweli na haki.

"Tunakabiliana na changamoto kama hizi, na changamoto hizi zinatupa Waislamu sote jukumu la kuionesha kwa uzito mkubwa sura na taswira sahihi ya Uislamu.

"Viongozi na wananchi wa Iran wana mtazamo chanya na wa karibu kuhusiana na wananchi wa Algeria na viongozi wa nchi hii. Tunatarajia kustawishwa uhusiano kati ya nchi mbili, kwa upande wa serikali na kwa upande wa mabunge, kutawezesha kustawishwa uhusiano katika nyanja za kiuchumi na kiutamaduni na pia kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu,"amesema.

Kwa upande wake, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, siku hizi Serikali za Magharibi zimekuwa zikieneza chuki dhidi ya Uislamu na kuwapiga vita Waislamu.

"Na wamewatusi Waislamu wote kwa kuichoma moto Qur'ani. Vilevile mashinikizo ya baraza jipya la mawaziri la utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina yameongezeka, lakini Wapalestina nao wametoa funzo kubwa kwa Wazayuni,"amesema. (parstoday)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news