Askofu Dkt.Shoo afunguka Mchungaji Dkt.Kimaro kupewa likizo, asisitiza uvumilivu KKKT

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt.Fredrick Shoo amewataka washarika wa KKKT Usharika wa Kijitonyama uliopo Dayosisi ya Mashariki na Pwani jijini Dar es Salaam kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho kunaonekana hali ya mvutano.

“Semina yetu ilikuwa ya wiki mbili, lakini leo niliitwa Ofisi ya Msaidizi wa Askofu na nilikuwa na kikao na Msaidizi wa Askofu na Mkuu wa Jimbo la Kaskazini, nimepewa barua ya likizo ya siku 60 na kuambiwa nirudi Machi 17 na nikirudi nikaripoti Makao Makuu ya Dayosisi,”alikaririwa Mchungaji Kiongozi wa kanisa,Dkt.Eliona Kimaro awali.

Dkt.Shoo ametoa wito leo Januari 17, 2023 ikiwa ni saa chache baada ya baadhi ya washirika wa kanisa hilo kuandamana kanisani hapo na kuuomba uongozi wa KKKT umrudishe Mchungaji Kiongozi wa kanisa,Dkt. Eliona Kimaro ambaye jana alitangaza kuwa amepewa likizo ya miezi miwili.

"Niombe utulivu kwa washarika na kwa Wakristo ambao wamesikia habari hizo za uamuzi amabao umefikiwa na Dayosisi yake. Tambua kuwa Dayosisi ina vyombo vyake vya maamuzi, na bila shaka jambo lenyewe linaendelea kufanyiwa kazi na dayosisi husika.

"Na sisi ambao sasa tunapokea taarifa kama hizi, tunaendelea kufuatilia na kupata taarifa zaidi kuhusu jambo hili ambalo linaonesha kuleta usumbufu na maitikio au reactions mbalimbali tofauti tofauti kutoka kwa watu mbalimbali,"amefafanua Dkt.Shoo.

Sakata la Mchungaji huyo kupewa likizo ya siku 60 bila sababu za likizo hiyo kuwekwa wazi limeibua gumzo mitandaoni ambapo, juhudi za DIRAMAKINI kuupata uongozi wa dayosisi hiyo zinaendelea ili kupata ufafanuzi.

Dkt.Kimaro amekuwa maarufu zaidi kupitia huduma za ibada ambazo amekuwa akiendesha ikiwemo Morning and Evening Glory: “The School of Healing: Shule ya Uponyaji”.

Ibada hizo huwa zinafanyika kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa kwa maana ya Morning Glory: Saa 11:30-12:30 Asubuhi, Evening Glory: Saa 12:00-2:00 Jioni.

Kwa mujibu wa ushirika huo, Shule ya Uponyaji ni mafundisho yenye msingi wa Kibiblia yenye lengo la kuwezesha watu wa rika na madhehebu yote kuponywa Kiroho, Kimwili, Kiakili na Kifikra kwa njia ya kumjua Mungu na kufahamu kusudi la Mungu kwa mwanadamu na kuishi maisha yanyoendana na kusudi la Mungu na viwango amavyo Mungu amevikusudia kwake.

Msingi wa Shule ya Uponyaji ni kutoka Methali 1: 1-7; ambao uanlenga kujua matendo makuu ya Bwana ili kujua hekima na adabu, kutambua maneno ya ufahamu, kufundishwa matendo ya busara katika haki, hukumu na adili, kuwapa wajinga werevu. Kuwapa vijana maarifa na hadhari, kuwaongezea elimu wenye hekima, na wenye ufahamu mashauri yenye hekima.

Shule hiyo ya Uponyaji inatambua umuhimu wa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla na kuwa vijana wengi wanahitaji kupewa maarifa na hadhari ili kuwajenga katika msingi ambayo itawasaidia kujituma katika kufanya maendeleo ambayo yataleta mabadiliko makubwa kwa Tanzania na Ulimwengu.

Mafundisho haya huwa yanalenga kuwasaidia vijana kupata maarifa ya kuona fusara zenye Baraka za Kimbingu na hadhari katika maisha yao.

Pia Shule ya Uponyaji huwa inaambatana na Ushauri wa Kichungaji unaofanyika kila mwezi Septemba lengo likiwa ni kutoa ushauri nasaha ili kuwafungua watu na kuponya jeraha zao, Majadiliano ili kutoa fursa ya kupokea shuhuda mbalimbali na kuona jinsi ambavyo watu wamefanikiwa ili kuwatia moyo wengine na kupata mbinu, ujuzi na maarifa ya kufanikiwa kupitia misingi ya Kibiblia.

Aidha, Shule ya Uponyaji huwa inawaleta watumishi wa kitheologia toka madhehebu mbalimbali, wachumi, wafanyabishara na wataalamu wa fani mbalimbali ili kuhudumia kanisa la Mungu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news