NA ADELADIUS MAKWEGA
KUNA wakati Shule ya Sekondari ya Ndanda ilijengewa bweni na Baba Abate wa Wabenediktine wa Ndanda ambalo lilijengwa kuokoa jahazi la bweni la wasichana la shule hii ambalo lilikuwa jirani na makazi ya watawa wa kike kutokana na uharibifu wa mvua kubwa za mwaka 1990.
Mvua hiyo ilileta madhara
makubwa na hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo
mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi kutembelea kukagua eneo hilo na kuwafariji
Watanzania waliokumbwa na madhara ya mvua hii na safari hiyo
ikasababisha kifo cha mwandishi wa habari wa Rais Mwinyi marehemu Habib
Halahala.
Kwa ambao hawamfahamu marehemu Halahala alichaguliwa na Rais Julius Nyerere kuzifanya kazi zake za Habari-Ikulu na kwa bahati nzuri Ali Hassan Mwinyi aliendelea kufanya kazi na Habibu Halahala.
“Siku ya msiba huo, Mzee Mwinyi alitumia usafiri wa helikopta, kuelekea Kusini mwa Tanzania, katika msafara huo alikuwepo pia ndugu Halahala. Walipofika eneo la tukio, Helikopta ilipotua tu miongoni mwa watu wa mwanzo kushuka ni Habib Halahala, yeye aliwahi kushuka ili kupiga picha ya Rais akishuka kwenye helikopta hiyo.
"Kwa bahati mbaya wakati anashuka panga za helikopta bado zilikuwa zinazunguka kwa kasi, bila kujua Habib hakuinamisha kichwa chake lile panga la helikopta likamkata shingo akafariki hapo hapo.”
Simulizi ya tukio hilo mwanakwetu aliikuta Shule ya Sekondari Ndanda miaka kadhaa baada ya kutokea.
Madhara ya mvua hizo yalikumba pia sehemu makazi ya watawa hawa Wabediktine likiwamo eneo la bweni la wasichana, ambapo baadaye watawa hawa waliokoa jahazi la ujenzi wake.
Ujenzi wa bweni hilo ulipokamilika kabla ya ufunguzi wanafunzi wa kike wa shule hii ya sekondari ya walihamishwa na kukaa katika mabweni hayo mapya ambayo yalijengwa pembezoni mwa shule hii kongwe.
Bweni hilo jipya liliongeza idadi ya mabweni kutoka mabweni ya awali ya Mawezi, Kibo, Mtandi na Ilulu ambayo ni mabweni tangu enzi za akina Benjamin Mkapa walipokuwa wanafunzi wa Ndanda.
Wakati ujenzi huo wa bweni la wasichana unakamilika mwanakwetu alikuwa mwanafunzi wa kidato cha sita. Maamuzi ya wakubwa wakati huo walisema kuwa mahafali ya mwaka 1998 yatumike kulifungua bweni hilo jipya.
Kabla ya mahafali hayo shule hii ilikumbwa na uhaba mkubwa wa walimu hivyo wanafunzi wengi waliochaguliwa kidato cha tano walihama, kwa hiyo walibaki wanafunzi wachache mno akiwamo mwanakwetu.
Katika kuhama huko waliondoka hata viongozi wa serikali ya wanafunzi akiwamo Kaka Mkuu. Kabla ya kufanyika mahafali uongozi uliokuwa unamaliza muda wake ulifanya mchakato wa kuwapata viongozi wanaoachiwa serikali ya wanafunzi na hoja kubwa ilikuwa kumpata Kaka na dada Mkuu ndani ya kikao hicho mwanakwetu alikuwapo.
Mapendekezo yalifanyika chini ya kikao kilichoongozwa na Dada Mkuu, kumbuka Kaka Mkuu alihama. Majina mawili yalipendekezwa vizuri na kujadiliwa huku maoni kadhaa yakitolewa na kikao hicho kikakubaliana bila shaka na kwa kauli moja jina la Kaka Mkuu mpya.
Mjadala ulihamia kwa mapendekezo ya Dada Mkuu jina lililopendekezwa lilijadiliwa kwa kina huku mwenyekiti wa kikao hicho-Dada Mkuu anayemaliza muda wake akipata changamoto kubwa kutoka kwa wajumbe juu ya jina linalopendekezwa.
Wajumbe kadhaa waliokuwepo katika kikao hicho wengi wakiwa na mawazo tafauti juu ya jina hio la Dada Mkuu mpya kwa kupingwa kwa jina la Dada Mkuu mpya lilitoa tashira mbaya kwa Dada Mkuu anayemaliza muda wake maana lilikuwa chaguo lake, kama vile wajumbe wanampinga Dada Mkuu na Mwenyekiti wa kikao hicho.
Madai ya wajumbe yalikua mengi dhidi ya jina hilo wakisema jina hilo lina tuhuma ya kujihusisha na mahusiana ya kimapenzi na baadhi ya walimu. Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa mkali mno akitaka ushahidi wa hoja hiyo kutoka kwa mjumbe aliyeibua jambo hilo.
Mjumbe alijibu kuwa kama tuhuma hizo ni za uwongo kwanini tuhuma hizo akubebeshwa mtu mwingine? Mbona jina lililopendekezwa kwa Kaka Mkuu hakuna tuhuma hata moja iliyotajwa? Mwenyekiti alikuwa mkali mno akisema mbona tuhuma hizo nzito mnawabebesha wasichana ambao ni dada na mama zenu?.
Mjadala ulipamba moto na mjumbe mmoja alisimama na kueleza ushahidi wake wa mazingira kadhaa aliyowahi kuyaona ya jina pendekezwa na mwalimu aliyetuhumiwa. Ushahidi huo ulimnyima raha Mwenyekiti wa kikao hicho lakini hakuwa na namna maana kikao hicho lazima kije na maamuzi yake.
Mwenyekiti alisimama na kueleza kuwa kuna watu wanakuwa wakali mno na kulikataa jina pendekezwa kwa hoja zisizo na ukweli, akiongeza kuwa jambo hilo siyo zuri kwanza wao wanahitimu kidato cha sita mwaka 1998.“Kwani wanaobaki hapa ni ndugu zenu? Acheni mambo yenu.”
Mjumbe mmojawapo aliinuka na kusema,“Hata wewe Mwenyekiti mwenendo wa tabia yako tunautilia shaka mno, hata wewe una shida hizo hizo zinazolalamikiwa kwa jina hilo pendekezwa, hatusemi mengi kwa kuwa unaondoka, tunatamani uondoke salama na wanaobaki wabaki salama na hiyo ndiyo nia ya maoni ya wajumbe kikaoni.
"Hatumchagui Dada Mkuu awe wakala wa kuwatoa usiku dada zetu na kuwapeleka mitaani, tunamchagua Dada Mkuu wa kuwalinda dada zetu hao wawe wa damu na hata hawa tunasoma nao pamoja.”
Kikao hicho kilijadili kwa muda na kwa bahati nzuri mwisho wa siku iliamuliwa Dada Mkuu awe binti mmoja wa Kidato cha Tatu aliyefahamika kama Bahati Gwambasa kumalizia muda hadi watakapofika kidato cha tano Julai 1998.
Kweli kikao cha walimu wa Shule ya Sekondari Ndanda kilikubaliana na hoja zote za maamuzi ya serikali ya wanafunzi na Bahati Gwambasa akawa Dada Mkuu.
Siku ya mahafali ilifika na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Nsa Kaisi alifika na kufungua bweni hilo na kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya shule hii ya sekondari ya umma nchini Tanzania.
Mahafali yalipokwisha kidato cha sita walifanya mitihani yao na kuondoka zao, wengine walipanda mabasi na wale Dar es Salaam akiwamo mwanakwetu walienda hadi Mtwara na kupanda boti na Dada Mkuu aliyemaliza muda wake na mwenyekiti wa kikao alipanda ndege kurudi kwao.
0717649257