NA MZALENDO HURU
SERIKALI ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan; imeendelea kutenga na kutoa fedha kwa uboreshaji wa miundombinu, ufundishaji na ujifunzaji katika shule za awali, msingi na sekondari.
Hivyo basi, walimu kama kioo cha jamii tuna kila sababu ya kuzingatia yafuatayo ili kuandaa vema taifa la kesho (wanafunzi wenzetu):
*Kusoma kanuni za utumishi
Tukizisoma, tukizielewa na kuzizingatia kanuni hizi muhimu za utumishi wa umma; zitatujengea uwezo mkubwa wa kufanya yafuatayo:
- Kutoa huduma bora
- Kuwa watii kwa Serikali
- Kuwa na bidii ya kazi
- Kutoa huduma bila upendeleo
- Kufanya kazi kwa uadilifu
- Kuwajibika kwa umma
- Kuheshimu sheria na taratibu
- Kujua matumizi sahihi ya taarifa
*Kutii Kanuni ya Mavazi sahihi
Ni vyema walimu wa kike na wa kiume kutii kanuni ya mavazi kwa kuvaa nguo zenye maadili na si zenye kudharirisha taaluma ya ualimu.
*Kutokuwa na utoro wa rejareja
Ni vyema walimu wa Tanzania tukawa na tabia ya kuwahi kufika kazini, kudumu kazini na na kuwajibika ipasavyo kwa wanafunzi wetu.
Tufanye biashara zetu baada ya muda wa kazi kumalizika badala ya kwenda kufanya biashara zetu nje ya taasisi zetu ndani ya muda wa vipindi.
*Kuepuka mahusiano/mapenzi
Sisi walimu ni walezi tuliominiwa na Serikali na wazazi wa wanafunzi. Hivyo, tusithubutu kujidharirisha na kuvunja usalama wa nchi kwa kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa wanafunzi tunaowafundisha; tusije tengeneza kizazi cha ukahaba.
*Kutoendekeza ulevi na mihadarati
Ni hatari sana kwa sisi kama walimu kuendekeza ulevi na matumizi ya mihadarati na dawa za kulevya bali; ni vyema tukawa mabalozi wa kuelimisha wanafunzi wetu na jamii juu ya athari za matumizi ya vilevi na mihadarati. Lengo ni kutopoteza nguvu kazi ya taifa.
*Kuwa waadilifu kwenye utumishi
Uadilifu ni moja ya tunda zuri na uhakika kwa ulinzi na usalama nchi. Lakini, ujeuri na ukaidi kwetu sisi walimu ni hatari sana kwa usalama wa taifa letu.
Hivyo, mara zote tuwe waadilifu wenye kuheshimu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utendaji kazi wetu na si vinginevyo.
*Kutokuwa wahujumu kwa Serikali
Serikali ni chombo muhimu kwa maendeleo ya taifa letu. Hivyo basi, si busara sisi kama walimu kujihusisha na hujuma zozote zikiwemo kuvujisha mitihani ya taifa na kuharibu shughuli muhimu za Serikali kama vile uchaguzi mkuu, sensa ya watu na makazi n.k Bali, tuwe waaminifu na wenye mapenzi mema kwa nchi yetu.
Baada ya maelezo hayo machache katika mengi, wajibu wetu mkubwa kama walimu kwa wanafunzi wetu ambao ndio taifa la kesho; ni kufanya mambo mazuri ili waige kutoka kwetu kwa kuyafanya maisha yao kuwa ya mfano kwa wengine. Aidha, tuwalee wanafunzi wetu:
(1) Kiakili (intellectually)
(2) Kimwili (Physically)
(3) Kiroho/Kiimani (Spiritually) na
(4) Kijamii (Socially)
Kwa kufanya hivyo, tutatengeneza kizazi chenye uzalendo, uadilifu, uwazi na uwajibikaji kwa taifa.