Fanyeni kazi kwa bidii-Dkt.Kisenge

NA MWANDISI WETU

WAFANYAKAZI wapya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma pamoja na maadili ya kitabibu ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wagonjwa kwa kufuata miongozi ya utoaji wa huduma za afya.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mafunzo elekezi kwa wafanyakazi wapya 57 walioajiriwa na Serikali kupitia Sektetariate ya Ajira na kupangiwa kituo cha kazi katika taasisi hiyo.

“Taasisi yetu imekuwa na hadhi ya kimataifa kwani hivi sasa inapokea wagonjwa kutoka ndani ya nchi pamoja na wagonjwa kutoka Afrika Mashariki na kati, hivyo kwa wadhifa huu naamini mtashirikiana na wafanyakazi mliowakuta kuendelea kuijenga taasisi hii.

“Nimatumaini yangu mtafanya kazi kwa bidii, kuwa na maadili kama ambavyo utumishi wa umma unavyotutaka kuwa na kuhakikisha hamuwi sehemu ya kuhamasisha rushwa ama kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa tunaowahudumia,”alisema Dkt.Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema Menejiment ya Taasisi hiyo itahakikisha wafanyakazi hao wanapata maslahi kutokana na utendaji wao wa kazi hivyo kuwataka kufuata mienendo ya wafanyakazi waliowakuta kazini.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wapya wenzake Daktari bingwa wa upasuaji Alex Msoka ameishukuru Serikali kwa kutoa ajira kwa waajiriwa hao na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata miongozo yote ya Serikali katika kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma za matibabu.

“Kama daktari nipo tayari kufanya kazi muda wowote, nilikuwa na shauku ya kufanya upasuaji wa moyo kwani ni eneo ambalo kwa sasa linakuwa sana hapa nchini hivyo kwangu mimi naamini nimekuja sehemu sahihi,”alisema Dkt. Alex.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Watoto wenye magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),Dkt. Sulende Khuboja aliwahimiza wafanyakazi hao kufanya kazi kwa kupendana kwani mahali pa kazi ni sehemu ambayo wafanyakazi hutumia muda mwingi wa kuishi.

“Wito wangu kwenu, fanyeni kazi kwa kushirikiana na kupendana kwani unapokuwa katika Taasisi hii unakuwa mmoja wa wanafamilia wa Taasisi hivyo upendo ni sehemu ya maisha yetu,”alisema Dkt. Khuboja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news