NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema uzinduzi rasmi wa Hifadhi ya Taifa ya Jozani Ghuba ya Chawa na Hifadhi Hai ni ufunguzi muhimu wa fursa nyingi zaidi za Kiuchumi, Kijamii na Kiikolojia hapa Zanzibar.
Mhe. Othman ameyasema hayo huko Jozani wilaya ya Kusini Unguja alipozindua rasmi Hifadhi ya Taifa ya Jozani Ghuba ya Chwaka na Hifadhi Hai, ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za kutimia miaka 59 ya Mapinduzi ya Zazibar.
Mhe. Othman ameitaka jamii wadau na washirika mbali mbali kuhakikisha kwamba hifadhi hiyo inalindwa ili iweze kutimiza malengo malengo ya kuisaidia Zanzibar kuongeza pato kutokana na sekta ya utalii kwa wegeni wengi kuweza kutembelea msitu huo .
Mhe. Makamu amesema kwamba, kwa mujibu wa wataalamu, Hifadhi Hai ina vigezo maalumu vinavyotumika kuteua eneo, ili kuingia katika Mtandao wa Hifadhi-Hai Duniani.
Amevitaja miongoni mwa vigezo hivyo kuwa ni kuwepo ushirikishwaji bora wa wananchi katika mipango na usimamizi wa Hifadhi ya Taifa na kuwepo Bayoanuwai za aina nyingi na adimu duniani ndani ya msitu husika pamoja na kuwepo mfumo mzuri wa kugawana faida na hasara miongoni mwa wadau wa Hifadhi husika.
Mhe. Othman amesema kwamba, kuna umuhimu kwa wadau na na Serikali kuhakikisha kuwa, kwa pamoja wanaendelea kuvisimamia na kuvilinda vigezo hivyo, kwa hali na mali, na kufuata maelekezo ya wataalamu.
Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawakumbusha wananchi kwamba, vigezo hivyo ndiyo misingi mikuu ya uanzishaji na usimamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Jozani-Ghuba ya Chwaka, hata kabla ya kujiunga na Mtandao wa Hifadhi-Hai.
Amesema kwamba Serikali kwa upande wake inaahidi kuvilinda na kuvisimamia, siyo kwa sababu ya UNESCO, bali kwa kuamini kuwa, ndiyo miongoni mwa Nguzo za Hifadhi ya Taifa ya Jozani-Ghuba ya Chwaka na Hifadhi Hai, ambapo pia uwepo wake ni faida kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amefahamisha kwamba kutokana na umuhimu wa kuwepo kwa Hifadhi hiyo sambamba na matakwa ya kisheria, Serikali ya Zanzibar imeona ni vyema kutangulia kuizindua na baadae kuendelea na taratibu nyingine za kiutekelezaji kwa faida ya nchi na jamii kwa jumla .
Aidha Mhe. Othman ametoa wito kuchukiliwa juhudi za ziada kuupandisha hadhi pia Msitu wa Hifadhi wa Kimaumbile wa Ngezi-Vumawimbi, ambao kwa kipindi kilichopita ulishidwa kupanda hadhi kutokana na mapungufu yaliyopelekea kukosekana kwa vigezo muhimu ya kupandisha hadhi hiyo.
Amesema kutokana na hali hiyo kunahitajika jitihada za makusudi, na Msitu huo wa Ngezi nao utimize vigezo muhimu vinavyohitajika ili hatimaye uweze kupanda hadhi ya kiwango cha Hifadhi Hai kama ilivyo Jozani.
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Maliasili Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis, amesema kwamba kuna jitihada kubwa zilizofanyika zilizosaidia kupatikana kwa hatua hiyo kuupandisha daraja msitu huo jambo linalochangia kuwepo ongezeko kubwa la wageni wanaotembelea hifadhi
Amefahamisha kwamba katika mwaka 2022 kuanzia Januari hadi Novemba, jumla ya wageni 52,666 wametembelea hifadhi hiyo na kuchangia kuingiza zaidi ya shilingi bilioni . 1.19 huku fedha za kigeni zilizokuswanywa zikiwa zaidi ya dola sitini na nane alfu.
Aidha amesema katika mwaka 2021, jumla ya wageni 58,902 walitembelea hifadhi hiyo na kuingiza kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni 56 ikiwa ni ada za kiingilio katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka huo wa 2021.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid Rashid, amesema kwamba mashirikiano ya wadau mbali mbali pamoja na kuwepo amani na utulivu nchini kumechangia mkoa huo kupata fursa ya kuwa na hifadhi hai baada yam situ huo ku8pandishwa daraja jambo linalochangia kuwepo idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo na kongeza mapato kwa wananchi na kupunguza ukali wa maisha.
Akisoma risala ya Ushirika wa Hifadhi hai Jozani ndugu Awesu Shaaban Ramadhan, amesema kwamba changamoto kubwa inayokabili ushirika huo ni pamoja na wanajamii kukosa, uelewa wa sera na sheria na hivyo kuendelea kufanya mambo yasiyokubalika katika eneo la hifadhi ikiwemo kukata msitu.
Awali Ofisa Ikolojia katika Hifadhi hiyo ndugu Habib Abdulmajid amesema kwamba msitu huo ni muhimu kwa kuendeleza biashara ya utalii Zanzibar kutokana na kuwa na vivutio kadhaa kwa watalii.
Amevitaja vivutio hivyo vya asili kuwa ni pamoja na kuwepo wanyama wengi adimu, ndege, miti na viumbe wengine ambao wamekuwa wakiwavutia sana wageni wengi kuja kutembelea msitu huo na kuchangia kuongeza mapato yatokanayo na biashara ya utalii nchini.
Tags
Habari
Hifadhi ya Taifa ya Jozani Ghuba Chwaka
Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu Zanzibar
Sekta ya Utalii Zanzibar