Huu hapa uchambuzi wa Kisimiotiki kuhusu Chawa

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

'CHAWA' ni msemo ambao umepata mashiko na matumizi mapana katika siku za hivi karibuni, licha ya kuwa ni neno ambalo limekuwepo katika Kamusi la Kiswahili Sanifu kwa muda mrefu.

Picha na fundselectorasia.

Neno au msamiati "Chawa" kwa sasa limekuwa ni msemo katika muktadha wa kisiasa na kiasi katika muktadha wa kijamii.

Msemo ni kipera au kijitanzu katika utanzu wa Semi ambao ndani yake mna vipera vingine kama methali, vitendawili, nahau, vitanza ndimi na simo au misimu.

Semi ni utanzu mmojawapo kati ya tanzu za fasihi simulizi huku tanzu nyingine zikiwa ni hadithi, Ushairi, Majigambo na Ngomezi. Hivyo, kitaaluma semi ni sehemu ya fasihi na msemo "Chawa" ni sehemu ya fasihi simulizi.

Kimsingi, nitachambua msemo "Chawa" unavyotumiwa kifasihi kwa kuongozwa na nadharia ya Simiotiki.

Hii ni nadharia inayohusika na uchambuzi wa matumizi ya lugha katika fasihi ikiwa na misimbo mitano.

Misimbo hiyo ni Kiseme, kihemenitiki, kiutamaduni, kimatukio na kiurejelezi. Nadharia hii inaitazama lugha kuwa ni muunganiko wa vitu viwili ambavyo ni kitaja na kitajwa.

Kitaja ni kile kinachotaja kwa mfano "chawa" na kitajwa ni kilichomo ndani ya "chawa" yaani kile kinachorejelewa.

Urejelezi unaweza kufanywa kwa namna mbalimbali lakini maana ya msingi ya kitaja ndiyo hutumika katika urejelezi.

Kiini cha Mada: Uchambuzi_ _wa_ _msemo_ _Chawa_

Kiini cha mada hii kimetokana na hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Januari 3,2023 kwa viongozi wa vyama vya siasa. Kauli hiyo ni hii hapa nanukuu:

_Uongozi_ _ni_ _ustahamilivu_, _yananipata_ _sana_. _Rais_ _Samia_ _anaweza_ _kustahamili_ _yanayosemwa_ _lakini_ _chawa_ _wako_ _na_ _chawa_ _wa_ _Rais_ _Samia_ _watagombana_. _Tufanye_ _siasa_ _za_ _kistaarabu_ _sio_ _za_ _kutukanana_.

Kauli hii ndiyo msingi wa uchambuzi wetu. Katika dondoo la nukuu hapo juu ni bayana kwamba neno hilo "chawa" limetumika kurejelea mashabiki au ushabiki kwa kiongozi na hapa kiongozi huyo anaweza kuwa ni Rais au kiongozi wa "chama cha kuonesha changamoto."

Kuanzia sasa Rais Samia ametupatia jina la vyama vya upinzani kuwa ni vyama vya kuonesha changamoto na siyo vyama vya upinzani.

Kimsingi, tunapotazama msemo "chawa" kisemiotiki na hasa kwa kurejelea msimbo wa kiseme ambao maana yake nasibishi ya kisemantiki ni ile hali ya chawa kuganda au kung'ang'ania katika mwili wa binadamu au kiumbe kingine kwa ajili ya kupata maisha au uhai.

Tunasema maisha na uhai kwa maana pana kwa sababu tumewahi kusikia watu wakifariki kwa sababu ya ushabiki wa kitu fulani. Raha ya chawa ni kupata hayo maisha na kifasihi sasa inavyotumika ni kwamba:

Mosi, mashabiki au wafuasi wa kiongozi au chama cha siasa wanafurahia na kuvutiwa na utendaji wa kiongozi wao na hawako tayari kuona au kusikia akibezwa.

Linapotokea hilo la kubezwa mashabiki hao wapo tayari kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hadhi ya kiongozi wao inaheshimiwa.

Pili, mashabiki wanakuwa na upendo wa dhati kwa kiongozi wao na wapo tayari hata kulala njaa na wakati mwingine kutandika kanga au aina nyingine ya vitandiko ili kiongozi wao apite. Ukivunja hadhi ya kiongozi huyo kwa bezo au kejeli chawa hawawezi kukubali.

Tatu, mashabiki au wapenzi wa kiongozi yeyote katika jamii hawapendi kusikia kiongozi wao anatukanwa matusi ya aina yoyote na ikitokea hivyo basi wanakuwa tayari kurudisha matusi hayo. Hivyo inakuwa ni kutukanana na siyo siasa tena.

Nne, mashabiki au chawa wanapenda unapomkosoa kiongozi wao basi useme amefanya mazuri yapi halafu ndiyo unasema "hata hivyo, pamoja na mazuri haya kuna upungufu kadhaa wa kadhaa ukifanyiwa kazi itakuwa ni sawasawa.

Hii "hata hivyo" ni kiunganishi muhimu sana katika kuwafanya chawa wa kiongozi fulani kujenga uvumilivu pale kiongozi wao anaposemwa kwa mrengo tofauti na ule wa imani yao kwake. Ni vema machawa wakazingatia kiunganishi hiki katika kujenga hoja zao.

Zaidi ya hayo, ni vizuri kuelewa kwamba "chawa" hapa ni wa pande zote na si kwa Rais pekee bali hata kwa viongozi wa vyama vya kuonesha changamoto nao pia wana chawa wao na hivyo hivyo nao hawatakubali kuona kiongozi wao mpenzi anasemwa vibaya.

Lazima watalipiza na ndicho hicho kinachosemwa na Rais Samia kwenye nukuu hapo juu. Hata katika ngazi za familia chawa wapo.

Hata katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi chawa wapo. Chawa wapo kila mahali kinachowatisha ni muktadha tu na hapo utapata aina fulani ya chawa.

Kwa mnasaba huo, chawa hata kwenye timu za mpira wa soka wapo na hapa Tanzania timu za Simba na yanga zina chawa wengi kuliko timu nyingine.

Hakuna chawa wa timu mojawapo anayekubali kushindwa pale inapokuwa ni katika kutetea timu yake. Chawa huyo atatafuta kila aina ya mbinu au maneno kuonesha kwamba timu yake ni bora kuliko nyingine.

Ubishani wakati mwingine hufika mbali mpaka wahusika kupigana na kudhuriana. Hivyo kwa kutumia msimbo wa kiseme unaweza kuelewa msemo "chawa" kwa maana pana ya kifasihi.

Pia, ukitumia msimbo wa kimatukio unaweza kuelewa vizuri zaidi msemo "chawa" unatumika kujenga dhamira au jumbe gani katika muktadha gani.

Hitimisho


Katika Insha hii fupi nimejaribu kuchambua msemo "Chawa" katika muktadha wa matumizi yake katika siasa na kama ulivyorejelewa na Mhe.Rais Samia kwenye hotuba yake kwa viongozi wa vyama vya kuonesha changamoto nchini Tanzania.

Kauli hiyo ya Mhe Rais Samia ililenga katika kusisitiza wahusika wote kufanya siasa za kistaarabu kwa masilahi mapana ya Taifa letu badala ya kufanya siasa zisizo na staha ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Msemo "chawa" kwa sasa umepata mashiko na matumizi mapana zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Hivyo, basi ni vizuri "chawa" wote wa vyama vyote kuhakikisha nao pia wanakuwa wanafanya uchawa katika amani na utulivu ili uchawa uendelee kutumika kwa nia nzuri ya kushindana kwa hoja zinazoliletea Taifa maendeleo.

Hoja ikitolewa na chawa wa upande fulani basi machawa wa upande mwingine wanajipanga kutafuta majibu ya hoja husika na siyo kutafuta matusi. Hapo kazi ya uchawa itakuwa nzuri sana.

-Insha_ _za_ _hamasa_ _ya_ _maendeleo_ _nchini_ _Tanzania_

MWANDISHI

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
5/1/2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news