NA FRESHA KINASA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji imetembelea mradi mkubwa wa maji wa Mugango-Kiabakri-Butiama unaojengwa katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara unaogharimu shilingi Bilioni 70.5 na kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na mkandarasi anayejenga mradi huo katika kuhakikisha unakamilika ili uwanufaishe wananchi wapatao 164,900 katika vijiji 39.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 14, 2023 Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Almas Maige amesema kuwa mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 73 hatua ambayo ni nzuri na inaleta faraja kubwa katika kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kumtua mama ndoo kichwani.
Maige amesema kuwa, kazi nzuri imefanywa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi za kukidhi miradi ya maji ukiwemo mradi huo wa Mgango-Kiabakari-Butiama ambao utakuwa na tija kubwa kwa wananchi katika kuchochea maendeleo ya shughuli mbalimbali za uzalishaji hivyo Rais anastahili pongezi nyingi za dhati kwa kuendeleza miradi hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Naye Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema kuwa mradi huo wa Mugango-Kiabakari-Butiama unaendelea vizuri na shabaha ya Serikali ni kuhakikisha unakamilika ili Wananchi waanze kunufaika nao.
Ameongeza kuwa, Wizara hiyo iko mstari wa mbele kuhakikisha miradi inayojengwa inaisha na kwamba Watanzania inawanufaisha kikamilifu kama ambavyo Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekusudia. Huku akibainisha Wizara imeendelea kutoa msisitizo kwa Watumishi kufanya kazi kwa kujituma na kuachana na mazoea kwa maslahi ya Wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof.Sospeter Muhongo amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa mradi huo ambao amesema utaondoa kabisa changamoto ya maji kwa Wananchi na maeneo unaokopita Wananchi watapata maji.
Prof. Muhongo amesema kuwa, Mradi huo unakidhi shauku ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alitamani mradi huo tangu mwaka 1974. Huku akiomba Wananchi kuutunza mradi huo na kuthamini juhudi za serikali kutekeleza mradi huo kwa ufanisi.
"Hapa zinatumika fedha za serikali na wafadhili, siku tunazindua hapa Rais alisema huu ni mradi mmoja unaenda kuwasaidia Wananchi kwa pamoja wote tena km 12 kila upande yatakuwepo matoleo hakuna haja ya kutoboa mambomba kwa Wananchi."
Akisoma risala hiyo meneja wa Mradi huo wa Mugango Kibakari Butiama, Mhandisi Cosmasi Sanda amesema utawanufaisha wananchi 164,900 na umegharimu dola za kimarekani milioni 24, 436,747 na umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania, BADEA na Saudi Fund. Huku mkandarasi anayejenga mradi huo ni UNIKI Construction Engineering Lesotho (PTY)LTD.
Amesema, tarehe ya kusaini mradi huo ilikuwa Novemba 17,2020 na muda wa utekelezaji wake ilikuwa siku 730 ambapo utekelzaji wa mradi huo hadi Januari 2023 ni asilimia 73. Kwa siku utazalisha lita milioni 35. na utahudumia vijiji 39.
Katika utekelezaji wa mradi huo amesema, kuna changamoto mbalimbali ambazo zinasababisha utekelzajai kuwa nyuma ya muda ikiwemo kujaa maji katika eneo la ujenzi wa chanzo na chujio hali inayosababisha kutumia mtambo wa kuondoa maji hayo wakati wote wa ujenzi.
Pia, kuongezeka kwa gharama za ujenzi kutokana na kuongezeka kwa kazi baada ya zoezi la uthibitisho wa usanifu uliofanywa awali na kuchelewa kuanza kutokana na mkandarasi kuhitaji kufanya uthibitisho wa usanifu kabla ya kuanza ujenzi kutokana na usanifu kufanyika muda mrefu uliopita.
Ameongeza kuwa, ili kuwezesha mradi kukamikika, wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kumuwezesha mkandarasi kumaliza ujenzi wa Mradi ili uanze kutumika kwa wakati ikiwemo uthibitisho wa usanifu unaendelea ambapo Mkandarasi amemalizia kazi ya uthibitisho katika mtandao wa usambazaji maji.
Pia mkandarasi amepata Mkandarasi Mwingine wa kusaidia kufanya uthibitisho na kujenga miundombinu ya mitambo ya umeme.