Kauli mbiu ya Wiki ya Sheria 2023 yawa kivutio Katavi

NA MWANDISHI WETU

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Katavi imezindua Wiki ya Sheria kwa mwaka 2023 huku mgeni maalum, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Pesambili Simuyemba akifurahishwa na kauli mbiu ambayo imekuja kwa muda muafaka hasa ukizingatia kuwa mkoa wake unayo migogoro mingi ya ardhi inayohitaji usuluhishi zaidi ili iweze kumalizika haraka, hivyo kuruhusu wadau kuendelea na shughuli za kilimo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umuhimu wa utatuzi wa Migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: Wajibu wa Mahakama na wadau”,
“Ninaipongeza sana Mahakama kwa kutuletea kauli mbiu hii inayoosisitiza umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumu endelevu.

"Kauli mbiu hii ni ya kimkakati kwa kuwa itachangia sana kumaliza migogoro mingi hasa ya ardhi ambayo ni mingi hapa mkoani kwetu. Mkoa wetu ni wa kilimo, hivyo kumalizika kwa migogoro kwa njia ya usuluhishi itakuza uchumi,” alisema.
Aidha, amemtaka Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mpanda Mhe, Gregory Rugalema kukutana na wenyeviti wa mabaraza yote ya ardhi mkoani Katavi ili kuweza kuweka mipango mahsusi kuona ni kwa namna gani kuli mbiu hiyo itawasaidia kupunguza migogoro ya ardhi.

Awali akitoa salamu zake za ufunguzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye amefafanua kwa kina maudhui ya kauli mbiu hiyo kwa kuzielezea faida nyingi za kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi.

Amesistiza pia kwa kuwataka wadau hasa Mawakili kuwa mstari wa mbele katika kuisimamia kauli mbiu hiyo kwa kuwa wao pia wamekuwa vinara wa kukwamisha usuluhishi pindi shauri linapokuwa linahitaji kumalizika kwa njia hiyo.

“Kauli mbiu hii ni muhimu sana kwa dunia ya sasa kwani kama mashauri mengi ambayo sheria zinaruhusu tuyamalize kwa njia ya usuluhishi yatakuwa na faida nyingi ikiwemo kuwa na jamii yenye amani, kupunguza mrundikano mahakamani, kuimarisha uchumi wa watu wetu na mengine mengi.

"Tatizo linabakia kwenu hasa Mawakili ambao mara nyingi mkienda kwenye usuluhishi mnarudi kusema umeshindikana,”alisisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news