Kemeeni maovu-Dkt.Mpango

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango amehimiza viongozi wa dini wakemee maovu katika jamii vikiwemo vitendo vya ubakaji, ulawiti, ukahaba, ushoga na ukatili kwa wanawake na watoto.

Dkt.Mpango amesema hayo Dar es Salaam wakati wa ibada ya kumsimika Philipo Magwano kuwa Askofu wa Dayosisi ya Pwani ya Kanisa la Afrika Inland Tanzania (AICT).

Amesema, kuna mmomonyoko wa maadili unaendelea kuongezeka katika jamii, hivyo akaomba viongozi wa dini waongeze nguvu kuilea nchi kimaadili kwa kukemea maovu yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na rushwa.

“Lakini pia kuna ndoa na mimba za utotoni na matumizi ya mavazi yasiyo na staha. Kuporomoka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya sana kwenye jamii na taifa letu na kunachangia sana kurudisha nyuma juhudi za kuharakisha maendeleo ya Tanzania,”alisema Dkt.Mpango.

Alisema, anaamni kama wananchi wakishika mafundisho ya dini maovu yatapungua na hata kuisha kabisa hivyo viongozi wa dini waisaidie serikali kujenga jamii yenye maadili mema hasa vijana.

“Wao ndio walengwa wa maovu yanayotendeka lakini pia wao ndio taifa la leo na kesho na warithi wa taifa letu.

“Kama tukiwaandaa vizuri mustakabali wa taifa letu na watu wake utakuwa kwenye mikono salama lakini tukishindwa leo tutalia na kusaga meno kesho na taifa letu litakuwa mashakani,” alisema Dkt.Mpango.

Pia aliomba viongozi wa dini wahimize waumini wao na Watanzania kwa ujumla umuhimu kufanya mazoezi na lishe bora hasa kwa wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Alihimiza wananchi wale vyakula vyenye virutubisho, matunda, mboga za majani, maziwa na vyakula vya asili.

“Nawaomba tuchukue hatua za makusudi kuhakikisha watoto wetu wanapata lishe bora ili tuwe na taifa lenye nguvu kazi ya watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri, kuleta tija katika kazi,” alisema Dkt.Mpango.

Aliomba pia viongozi wa dini watumie nafasi yao kuhimiza usafi na utunzaji wa mazingira kwa kukemea ukataji ovyo miti na wahamashe kupanda miti rafiki wa maji na ya biashara na ya dawa na maua kupendezesha maeneo ya kuishi.

Dkt.Mpango aliomba viongozi wa dinia waendelee kuiombea nchi amani na wawahimize waumini hasa vijana wafanye kazi kwa bidii kwa kuzitumia fursa zilizopo kikiwamo kilimo cha mboga mboga, ufugaji wa kuku, wanyama, nyuki na wadudu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news