NA ADELADIUS MAKWEGA
JANUARI 15, 2022 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko kwa baadhi ya nafasi zake na kuwachagua wanachama wake kadhaa katika nafasi hizo akiwemo mzee wetu Mizengo Pinda ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa hakika Mizengo Pinda ni jina kubwa miongoni mwa wana CCM aliyejipambanua kama mtoto wa mkulima tangu alipokuwa Naibu Waziri wa TAMISENI wakati huo wizara hiyo ikiongozwa na Brigedia Hassan Ngwilizi, huku Mizengo Pinda akiwa miongoni mwa wana CCM wachache waliowahi kufanya kazi na Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Mrisho Kikwete na John Pombe Joseph Magufuli na sasa Samia Suluhu Hassan ndani ya chama na serikali.
Katika hili, yapo majina yaliyopigwa mkasi na kutajwa majina mapya ikiwemo nafasi ya Katibu wa Ikitikadi na Uenezi Taifa na joho hilo kuvishwa ndugu Sophia Mjema aliyewahi kuwa kada wa CCM kabla ya kuwa mkuu wa wilaya ya Lushoto na sasa anakabidhi ukuu wake Mkoa wa Shinyanga na kuingia jikoni katika upishi wa propanganda za chama hiki cha siasa.
Orodha ya makada wa CCM waliowahi kushika nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa ni ndefu, miongoni mwao ni Moses Nnauye, Kingunge Gombale Mwiru,Omar Ramadhani Mapuri, John Mgeja, Jackson Msome, John Chiligati, Nape Nnauye, Humphrey Polepole, Shaka Hamdu Shaka na sasa kasia li mikononi mwa Sophia Mjema.
Miongoni mwa majukumu ya idara hiyo ni kufanyia kazi na kueneza masuala ya itikadi na Sera za CCM, kupanga na kusimamia mafunzo na maandalizi ya makada na wanachama na kusimamia vyombo vya habari vya chama, mawasiliano na uhamasishaji wa umma.
Pia idara hii inawajibika kuongoza na kusimamia maandalizi ya sera, programu na ilani za uchaguzi za CCM pamoja na kusimamia utafiti, maktaba na nyaraka za chama hicho kikongwe.
Wana CCM walioshuhudia Ukatibu Uenezi wa Moses Nnauye wanamtaja kuwa alifanya kazi kubwa aliposimamia kutungwa kwa nyimbo kadhaa za chama hiki na kuweza kuzunguka na makada mashuleni na vyuoni wakisomesha elimu ya siasa, mathalani baadhi ya watu wakiutaja wimbo huu,“Sisi tumekwisha uwasha mwenge, tumekwisha uwasha mwenge, nakuuweka juu ya mlima, milima Kilimanjaro… Kuwasha mwenge, kuwasha mwenge na kuuweka Kilimanjaro.”
Wimbo huo na nyimbo nyingi za itifaki ya CCM zkitungwa na marehemu Moses Nnauye mwenyewe, kulithibitisha hilo ukitembelea maktaba ya TBC Taifa (RTD) utalihakikisha hilo. Katika hili ndiyo kusema Moses Nnauye alikuwa na ujirani mkubwa na waandishi wa habari na watangazaji wa wakati huo ndiyo maana alifanikisha zoezi hilo lenye ushahidi milele.
Huku naye Kingunge Gombale Mwiru alikuwa na uwezo mzuri wa tafsiri ya sera, Imani na itikadi ya CCM kwa wananchi wake na uhalisia ukoje.Hilo linathibitishwa na Kingunge hadi umauti unamfika aliendelea kufanya tafsiri ya hilo japokuwa cheo hicho hakikuwa katika mikono yake tena.
Mwanakwetu huko kuelezea chama kinaamini nini, kuzungumza habari za chama na wanahabari, kutumiwa nyimbo katika kazi na mkutano ya chama kupanga hiyo mikakati huko ndiko kufanya propaganda za chama na jambo hili kwa kilatini wanaita Propaganda Fide.
Kumbuka kuwa mambo hayo lazima yawe katika mwongozo maalumu unaokwenda na kalenda maalumu na kila siku unatakiwa kuwa na jambo jipya ukitumia vikao, mikutano mafunzo na vyombo habari kama vile mitandao ya kijamii, magazeti, runinga, redio na kadhalika hapa unatakiwa kujua pia lile linalofanyika Mbeya ndiyo liwe sawa na linalofanyika Mwanza vile vile.
Kwa kuutazama wasifu wa Bi Sophia Mjema yeye ni mtaalamu wa mifumo ya kompyuta. labda hilo litasaidia yeye kuweka hiyo mifumo vizuri lakini ndani ya hilo kuna maswali mengi kipi kinachokwenda katika hiyo jamii ya wana CCM na Watanzania katika hiyo mifumo?Je kinapelekwa kikiwa kimefinywangwaje? Lakini propaganda vile vile ni kuileza jamii kinachofanywa na CCM Je Sophia Mjema anapofanya hivyo je jamii inamuonaje?
Ukiitishwa mkutano wa CCM je wapinzani na wana CCM watavutiwa na uwepo wa Sophia Mjema na maelezo yake katika mkutano huo bila ya kujali cheo chake ?
Je ndugu Sophia Mjema uwezo wake wa kucheza na maneno ukoje? Je anauvumilivu upi pale anaposhambuliwa moja kwa moja yeye binafsi ?
Ashakumu si matusi tilia maanani kisa hiki,
“Wanaweza kusema huyu ni mzinzi, huyu anapenda sana mapenzi, sasa jamani nisipopenda mapenzi nitakuwa mtu wa namna gani? Si ndiyo maana nilioa? Nikafunga safari hadi kwa Paroko na mke wangu, nikaoa, jamani hili nifanyeje? Jamani nimeoa hili niyatumikie vizuri mapenzi, ndiyo maana nilioa hili niyatumikie vizuri mapenzi (watu wanacheka) Jamani kuna matusi mengine ni ya kawaida kabisa, jamani chapeni kazi.” Maneno haya na ndugu Albart Chalamila maelezo haya ni sayansi ya juu ya siasa sayansi kubwa sana ya kujenga hoja zenye mvuto kwa hadhira.
Je? majibu ya maswali haya yanaonekana katika wasifu ndugu Sophia Mjema?Hilo mwanakwetu ameliona ni changamoto kubwa tangu Shaka hamdu, Humprey Polepole, na hata Nape Nnauye.
Katika mikutano ya kuomba kura akisimama jukwaani uwepo wake unaweza kuiongezea CCM kura?
Tilia maanani kisa hiki, “Asalaam aleikuum ! Mambo! (poa) CCM Oyee (Manara huyu, Manara huyu, Manara huyu wana CCM wanasikika wanaimba wakishangilia uwepo wake) Jamaani nilipofika hapa nimeulizwa mbona sijavaa nguo za chama?(ndiyo) Mbona sijavaa nguo za chama? Jamani ndugu yenu nimetoka safari, nimetoka safari, nimefika moja kwa moja hapa mkutanoni (sawa) Wote mnafahamu kuwa chama kipo ndani ya moyo wangu (moyoniiii…).
"Kwa kuwa leo ni mkutano wa Katibu Mkuu wa Jumuiya yetu ya Wazazi, kwa kuwa tuna mikutano mingi ya kampeni tutakuja kusema mengi, Wana CCM wenzangu wa Ilala ! La kwanza huwa tunakawaida ya kujiamini saaana hatuendi kupiga kura siku ya uchaguzi, tuna kawaida ya kuona kwamba tutashashinda, tunakawaida ya kuona diwani kesha kuwa diwani, Zungu keshakuwa mbunge na Rais keshakuwa Rais hilo tunakosea sana, siku ya uchaguzi twendeni tukapige kura,ukisema fulani keshaenda mie siendi kura zitapungua…” Huyu ni Haji Sunday Manara walipomshitukiza tu kuongea katika mkutano huo wa kampeni za CCM na wala hakusita kujibu swali la sare hadharani huku umati ukimshangilia sana.
Kwa maelezo hayo mwanakwetu anaamini kuwa Albart Chalamila na Haji Manara ndugu hawa wawili wanaweza kuwa majina sahihi hapo baadaye kuifanya kazi hii ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM Taifa. Kwa heshima na taadhima mwanakwetu anampongeza sana ndugu Sophia Mjema kuchaguliwa katika nafasi hiyo
Kwa heri
0717649257