NA OR-TAMISEMI
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu,Dkt. Charles Msonde ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa kwa ajili ya kuwapokea kidato cha kwanza kwa mwaka huu 2023.
Akiwa wilayani hapo ameonesha kuafurahishwa na kuona namna halmashauri hiyo walivyotumia fedha walizopata kikamilifu kwa kujenga shule mbili za sekondari kwenye maeneo ambayo wanafunzi walitembea umbali mrefu kufuata shule ya sekondari.
Dkt.Msonde alitemebea shule mbili za sekondari ambazo zimejengwa kwa fedha zilizotolewa na Serikali Kuu ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya kupokea kidato cha kwanza mwaka huu.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Ihanda alikagua madarasa matano yaliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 100 yakiwa kwenye hatua za ukamilishaji tayari kupokea kidato cha kwanza, 2023.
Pia alitembelea shule mpya ya Sekondari ya Masena ambayo pia imejengewa madarasa matano na ipo tayari kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza,2023.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt.Msonde ameridhishwa na ujenzi wa madarasa katika shule hizo ambazo zitawapunguzia wanafunzi adha ya umbali mrefu kufuata shule.
“Nakumbuka wakati tumepata fedha hizi, viongozi wa Kongwa waliomba mjenge shule kutoka kwenye fedha tulizopewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na tukaridhia, sasa leo nilikuja kuona hizo shule, kwa hakika nimeridhika na naridhia shule hizi kuanza mara moja," alisema Dkt.Msonde.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remedius Mwema Emmanuel amesema kuwa, shule hizo zilishapangiwa wanafunzi na maandalizi mengine yote yamekamilika kwa shule kufunguliwa.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa fedha hizi pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kuridhia tuweze kuanzisha shule kwa fedha za madarasa tulizopewa.
"Shule hizi ni msaada mkubwa kwa wananchi wetu na kwa ile ya Ihanda itachukua wanafunzi kutoka vijiji vya Ihanda, Masinyeti na Vihingo na ile ya Masema itachukua wanafunzi toka Masena, Kilimani na Songambele,"amesema Mkuu huyo.