Mandonga:Ninarudi Nairobi kumzika mtu chapu, nitakuja na ngumi nyingine si Sukunyo tena

NA DIRAMAKINI

BONDIA Mtanzania Karim Mandonga ameahidi kurejea tena Jamhuri ya Kenya ifikapo Aprili, mwaka huu kwa ajili ya kwenda kumzika mtu chapu.

Mandonga maarufu kama Mtu Kazi ameyasema hayo usiku wa kuamkia Januari 15, mwaka huu baada ya kutumia muda wake vema kumchakaza mpinzani wake Daniel Wanyonyi katika ukumbi wa Tsavo Ballroom KICC jijini Nairobi.
Ushindi wa Mandonga ulikuja baada ya Wanyonyi kukubali kushindwa raundi ya sita katika pambano la raundi 10 ambapo hakutaka kuendelea na pambano na kukubali kuwa Mandonga ndiye mshindi.

"Anataka anapigwa, hataki anapigwa, ndiyo nimeweka uthibitisho huo kwa Wakenya. Kwamba anataka anapigwa, hataki anapigwa. Ngumi imetoka Ukraine kaka, kwenye mlipuko wa mabomu, hii ni Sukunyo lazima ifanye kazi kokote kaka.

"Sasa ninarudi tena Kenya, ninakwenda Tanzania, mwezi wa nne ninarudi tena Nairobi kumzika mtu chapu,raundi ya kwanza kaburi lake lipo wapi, ninamzika chapu, nitakuja na ngumi nyingine na si Sukunyo tena,"amesema Mandonga.
Pia ameonesha moyo wa shukurani kwa mashabiki wa Kenya na wadau mbalimbali nchini Kenya na Tanzania kwa kumuonesha upendo mkubwa wakati akitimiza majukumu yake hayo.

Wanyonyi, bingwa wa zamani wa Umoja wa Ndondi wa Afrika (ABU) alibaki kwenye kona yake wakati kengele ya raundi ya sita ilipolia na kumlazimisha mwamuzi wa pambano Julius Odhiambo kutangaza Mandonga kuwa mshindi kwenye mtoano wa kiufundi.

Baada ya raundi mbili za kwanza zilizokuwa zikishindaniwa kwa usawa,Mandonga aliendeleza mchezo wake katika raundi zilizofuata kwa kuangusha makonde ya Sokunyo ambayo yalionekana kumzidi nguvu mpinzani wake raundi ya nne na ya tano.

"Nilikuambia nilikuja hapa kwa ajili ya biashara nzito na Wanyonyi, na amehisi nguvu za vipigo vyangu," Mandonga alisema baada ya kushinda pambano hilo katika onyesho hilo la Solid Rock Promotion.

"Nataka kuwashukuru mashabiki wangu wote kutoka eneo hili na hasa Kenya kwa sapoti yao, nilijihisi kuwa nyumbani na lilikuwa tukio la kushangaza," Mandonga alisema.

Mike Odongo wa Solid Rock Promotion alikadiria idadi ya mashabiki zaidi ya 2,500. "Tulifunga mauzo ya tiketi kufikia saa saba usiku na watu bado waliomba zaidi," alisema Odongo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news