MHESHIMIWA HAKIMU MGENI

NA ADELADIUS MAKWEGA

“Jamani msinunue mikate ya duka lileee ! Kwa kuwa yule jamaa anatumia miguu yake yenye matende yanayotoa usaha kukanda ngano kutengenezea mikate hiyo inayouzwa katika bekari yake.”

Haya yalisemwa na wanakijiji kimojawapo katika Wilaya ya Bagamoyo wakati huo ambacho sasa ni eneo lenye maendeleo ya kutosha kutokana na wananchi wengi kujikita katika shughuli zao za biashara na kilimo.

Bwana Hassani ambaye ni marehemu hivi sasa alimiliki bekari kubwa iliyokuwa inaoka mikate wakati huo.

Shida ya ndugu Hassani alipatwa na ugonjwa wa matende na miguu yake ilivimba kidogo kidogo na hadi kujaa hilo likampa tabu mno hata kushindwa kutembea umbali mrefu.

Mwanakwetu tambua kuwa maishani majina yanabadilika kwa sababu mbali wengine wakitoka jandoni, wengine wakivunja ungo, wengine wakibatizwa, wengine wakibadilisha dini, wengine kazi wanazofanya, wengine tabia zao na wengine ugonjwa.

Ndugu Hassani alipachikwa jina la Hassani Bini Matende kwa kuwa alifikwa na ugonjwa huo.Ugonjwa huo ulisababisha Hassani abatizwe jina jipya lakini jina lake halisi lilikuwa ni Hassani Bini Ali.

Je Hassani alikasirika? La hasha hakuuomba kwa Mola ugonjwa huo, ulimjia tu kwa matakwa ya Mola mwenyewe.

Hali ya ugonjwa huu ilisababisha Hassani Bini Matende biashara zake ziyumbe-huku watu wakisema kuwa sasa atatoka katika utajiri na kuwa fukara ngoja tumuone Hassan Matende fukara.

Mke wa ndoa alimkimbia kukwepa aibu hiyo. Kama mke aliyemtoroka Hassani Bini Matende angeweza basi angeibeba na bekari hiyo na kuondoka nayo lakini hiyo ni mali isiyohamishika.

Wawili ni wawili na mmoja ni mmoja tu, kazi zilimuelemea ndugu Matende alishindwa kufanya biashara zake vizuri.

Wanakijiji sasa walianza kuikwepa bekari hii na kwenda kupata huduma hiyo mbali kuhofia maneno ya usaha wa Hassani Bini Matende kutoka katika ugonjwa huo.

Pengine wanakijiji hawa walifanya huo unyanyapaa bila ya kujua kuwa kile kinachosemwa kuwa ni kweli au uongo, lakini Hassani Bini Matende yalimifika.

“Je ninafanyaje kuweza kuokoa uhai wangu? Maana sasa hali ya ugonjwa huu na miguu yangu inazidi kuvimba, nikishindwa kutembea, miguu yangu ikiwa mizito mithili ya mawe ya mizani ya kilo tano tano yamepachikwa katika nyao zangu? ” Hassani Bini Matende alijiuliza akilini mwake.

Hassan Bini Ali ambaye alikuwa Muisilamu mshika dini yake vizuri hata alipokwenda kusali msikitini aliamua kukaa mstari wa mwisho kabisa ili asiharibu ibada ya wanzake waliofika kusali hapo.

Mwezi wa kwanza ulipita, hali ilikuwa hivyo hivyo, hadi mwezi wa sita akitafakari namna ya yeye kuweza kuishi. Hapo alijipa majibu kuwa lazima amtafute msaidizi au aoe mwanamke mwingine.

Hassani Bini Matende alizidi kuwa njia panda, swali lingine likamjia je atampata wapi mwanamke atakayeweza kuishi na mtu mwenye matende? Kijiji hapo sasa vijiji vya Ujamaa ndiyo vilikuwa vimepamba moto, huduma mbalimbali zilikuwa zinapelekwa kama vile shule, zahanati na mahakama. Kijiji kilipokea watumishi wageni kutoka bara na pwani kwenda kujenga Ujamaa wa Julius Nyerere.

Muda wote huo, wateja waliendelea kupungua katika bekari yake lakini wapo wateja wengine ambao hawakutilia maanani yale maneno yaliyokuwa yanasema hasa hasa watumishi wa serikali wao waliendelea kuwa wateja wa Hassani Bini Matende kwa hoja mbalimbali, wengine wakiona kuwa yaliyokuwa yanasemwa yalikuwa uongo na wengine walishindwa kwenda kupata huduma mbali na hapo kwa hiyo vijiji vya jirani kwa sababu ya kubanwa na majukumu ya kazi.

Kumbuka ujamaa ukaboresha mahakama, shule na zahanati huku watumishi wakiongezeka kutoa huduma hizo, katika hilo alipelekwa hakimu kuamua mashauri yaliyokuwa yanapelekwa katika mahakama.

Hakimu huyu alifanya kazi vizuri na kusaidia sana kupunguza migogoro yote iliyokuwa inapelekwa kwake akifanya maamuzi ya haki bila ya upendeleo wowote ule.

Jina la hakimu huyu lilienea na kusambaa katika kila kijiji jirani kutoka na maamuzi yake ya haki mahakamani.

Jambo hilo lilisaidia kusafisha majina ya mahakimu wabaya waliokuwa wakilalamikiwa kwa uonevu wa maamuzi yao.Watu wakiwa mashambani wakilima walimtaja hakimu huyu na kumuombea mema na uhai mrefu na huku wakiyataja majina ya mahakimu madhalimu na kuwaombea mabaya yakisindikizwa ba laana kadhaa.

Kila jioni hakimu huyu mwema akitoka kazini alipitia kwenye bekari ya Hassani Bini Matende na kununua mkate wake ambao alikuwa akiutumia kama kifungua kinywa.

Hiyo ilikuwa desturi, huku baadhi ya watumishi wa mahakama wenyeji wakimwambia hakimu huyu binti shida ya bekari ya Hassani Bini Matende, lakini maneno hayo hakimu huyu hakuyaelewa kabisa.

Hassani Bini Matende alimzoea hakimu huyu mno kama mteja na mfanyabiashara kwa muda mrefu. Hassan Bini Matende akisema, “Karibu dukani mheshimiwa hakimu mgeni.”

Ujirani huu ulisababisha Hassan Matende awe anamtengenezea na kumuuzia mkate ulio mithili ya keki hakimu huyu mgeni kwa bei ya chini bila ya hakimu kufahamu hilo.

Jambo hilo la kwenda kununua hapo watumishi wenyeji wa mahakama wakasema hakimu mgeni kalogwa na mikate ya Hassani Bini Ali.

Siku moja Hassani aliamua kusema la moyoni baada ya kuvutiwa na mama huyu msomi wa sheria. Msomi huyu wa sheria aliyasikiliza vizuri maneno ya mahaba ya Hassani Bini Matende na kumpa jibu kuwa ngoja kwanza akalitafakari jambo hilo na jibu litatolewa.
Hassani Bini Matende alivyoambiwa hivyo aliamini kuwa jambo hilo lishaharibika kwa kuwa kama hakimu huyu atauliza taarifa zake maelezo ya ugonjwa wa wake yatamfikia hakimu huyo lakini alijipa moyo kuwa kama hakimu huyu aliendelea kula mikate ya dukani kwake basi ombi lake litakubaliwa tu.

Hali iliendelea hivyo na mikate ilinunuliwa kila siku sasa Hassani akikataa kupokea pesa ya mheshimiwa hakimu naye mheshimiwa hakimu akimwambia kuwa akifanya hivyo anakosea sana, kwa hiyo Hassani Bini Ali aliendelea kupokea pesa za mheshimiwa huyu dukani hapo.

Baada ya miezi mitatu mheshimiwa hakimu alikubaliana na maombi ya Hassani Bini Ali wakafunga ndoa wakawa mke na mume pika pakua.

Maneno yalizidi inakuwaje mheshimiwa hakimu mrembo anaolewa na Hassan Bini Matende? Hilo lilikuwa gumzo kubwa Bagamoyo nzima, lakini ndiyo hivyo tena ubani umeshachomwa na ndoa imekamilika, nyie semeni hakimu yupo katika himaya ya Hassani Bini Matende.

“Kila asubuhi hakimu akiamka alikusanya nguo za mumewe anazifua vizuri na kuzianika na kumvisha mavazi masafi na baadaye kuelekea kazini.” Majirani na vibarua wa bekari hiyo walisimulia hilo.

Kazi ya usafi ilikuwa ya kila asubuhi na kila jioni, huku ndugu wa mheshimiwa hakimu waliokuwa wanatoka mashambani waliposikia habari hiyo dada yao aliolewa n mtu mwenye matende waligawanyika katika makundi mawili wapo walichukia mno na wengine wakisema hayo ni maamuzi yao wapendanao.

“Mie nitakwenda lakini kama akituandalia chai ya maziwa yaani ninahisi kama ninakunywa chai ya usaha wa matende ya mumewe.” Ndugu wapingaji walisema kwa dhihaka kubwa.

Kumbuka Hassani Bini Matende alikimbiwa na mkewe wa kwanza na nduguze, huku wengine kuiba mali zake na kutokomea kusikojulikana.

Huyu mkewe hakimu ndiyo alikuwa tegemeo kidogo kwa Hassan Bini Ali sasa akawa anaonekana nadhifu.

Hali ya ugonjwa huu wa matende na kutengwa kwake ilizidi kuwa mbaya, alipatiwa huduma hapa na pale huku kijijini wakisema kuwa hakimu wao yupo bize na matende ya mumewe tu na kazi haifanyi vizuri.

Baadaye Hassani Bini Matende aliugua mno na aliamua kuandika wosia juu ya mali zake kadhaa ambazo nyingi zilikuwa hazifahamiki wazi wazi sehemu kubwa aliamua kumuachi mkewe huyu hakimu na wakfu katika msikiti aliokuwa anasali.

Kwa bahati mbaya Hassani Bini Ali hakuwa na mtoto na mkewe wa kwanza na hata mtoto na mkewe hakimu.

Baada ya kuandika wasia huo Hassani Bini Ali alifariki dunia. Waamini wenzake waliuchukua mwili wake kuuosha na kumsalia na baadaye kumzika huku mali zake ziligawanywa kama sheria ya dini yake na wosia wake ulivyoelekeza.

Sehemu ya mali zake alizoacha kama wakfu kwa msikiti kando ya nyumbani kwao mali hizo zilitumika katika shughuli zote za dini ya Kiisilamu.Mama huyu ambaye sasa ni hakimu mstaafu ni mfanyabiashara mkubwa na hakichukua bidhaa ng’ambo ya Tanzania na kuuza bara na visiwani.

Mwanakwetu nduguze mheshimiwa hakimu huyu wale wakataa chai ya maziwa ya Hassani Bini Matende sasa wanainywa vizuri chai ya maziwa nyumbani kwa Hassani Bini Ali ambaye ni marehemu wakisahau hata maneno yao dhidi ya mume wa ndugu yao.

Unaweza kujiluliza Je! mama huyu hakimu aliamua kuishi na Hassani Bini Matende kutokana na fedha, mapenzi au huruma? Mwanakwetu swali hilo ni unyanyapa tu.

Kubwa la kujifunza unyanyapaa siyo jambo zuri na katika maisha kila mmoja wetu anayo matende yake yaweza kuwa maradhi,fitna, kiburi, chuki, choyo, dharau, utajiri au umasikini, basi ni vizuri kuvumiliana kwa kila hali.

makwadeladius@gmail.com
0717649257.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news