Mheshimiwa Mchengerwa asema Serikali imedhamiria kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili

NA JOHN MAPEPELE

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imedhamiria kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili ili kukuza na kubidhaisha lugha hii adhimu duniani.
Mhe. Mchengerwa amesema haya leo Januari 25, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akimkaribisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuhutubia kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo ya Kiswahili.

Amesema, hivi sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazokua na kuenea kwa kasi kubwa ulimwenguni ambapo Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa kumi duniani. Hivyo, kasi ya ufunzaji na ujifunzaji wa lugha hii imekuwa ikiongezeka kila uchao.
Aidha, amesema Kiswahili ni lugha ya mawasiliano mapana katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa upande wa Tanzania licha ya kuwa lugha ya Taifa ndiyo lugha kuu ya mawasiliano.

Amefafanua kuwa,lugha ya Kiswahili kwa sasa imevuka mawanda ya kuielezea lugha yenyewe na hivyo inatumika kuelezea taaluma mbalimbali kama vile afya, kilimo na sheria.

Amesema Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali kwa kuzingatia kwamba Kiswahili ni kiunganishi muhimu cha jamii mbalimbali ndani na nje ya Tanzania na kwamba lugha hii inaeleweka na watu wengi mijini na vijijini.
"Lugha ya Kiswahili inawaunganisha Watanzania ambao wako katika makabila zaidi ya 150. Watanzania hawa wanaishi kwa ushirikiano na uelewano kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Haishangazi kwa mfano kumwona Mtanzania kutoka mkoa mmoja akiishi na hata kuoa au kuolewa katika mkoa mwingine bila kipingamizi chochote kwa kuwa watu hawa wanaunganishwa na lugha ya Kiswahili,"ameongeza Mhe.Mchengerwa.

Kutokana na kupanuka kwa matumizi ya Kiswahili ni dhahiri shairi kwamba hata ndoto zetu mara nyingi tunaota kwa Kiswahili.Ndugu Mgeni Rasmi, Wizara ninayoiongoza mbali na mambo mengine imepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba lugha ya Kiswahili inakua na kuenea kwa kasi inayotakiwa.

Amepongeza uamuzi wa kampuni ya ALAF wa kuwekeza katika lugha ya Kiswahili ambapo mbali na kutoa tuzo pia inatoa ufadhili kwa wanafunzi wa Umahiri Katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili na amezitaka kampuni nyingine kuiga mfano huo.
Aidha, amemhakikishia Mhe. Waziri Mkuu kuwa Wizara yake itaendelea kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na viongozi wakuu ili kukuza lugha ya Kiswahili.

Pamoja na maelekezo mengine, Mhe. Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kuanza kutoa Tuzo maalum za Kiswahili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news