NA DIRAMAKINI
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Butiama mkoani Mara, Mheshimiwa Jumanne Sagini amewataka viongozi wa Kijiji cha Nyabange wilayani humo kushirikiana na wananchi wao kukamilisha ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na matundu ya vyoo ili shule hiyo mpya iweze kupata usajili na kuanza kupokea wanafunzi.

Akizungumza mara baada ya kukagua shughuli za ujenzi zinazoendelea shuleni hapo, Sagini amesema kuwa siri kubwa inayopelekea miradi kuweza kufanikiwa na kukamilika kwa wakati ni viongozi kuhakikisha wanawashirikisha wananchi na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu hatua zinazofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo kwa kuwa na uelewa wa pamoja na wananchi kuweza kuwa na umiliki wa miradi.
“Kazi mnayoifanya ni kwa niaba ya Wananchi. Sisi tumekabidhiwa haki ya kusimamia hivyo inatupasa tutoe taarifa kwa wananchi waliotutuma. Ukiimarisha mawasiliano endelevu kati ya unaowaongoza na viongozi unajenga uaminifu. Huwezi kuwaita kesho wakakuangusha lazima watakuunga mkono. Ukiwakwepa wananchi na ukajimilikisha mradi wewe kiongozi ni tatizo kubwa,”amesema Mheshimiwa Sagini.

Pia, ni sababu kubwa ya kutowafanya wanafunzi wengi kutomaliza masomo yao ya kidato cha nne na kufanya vizuri ikichangiwa na umbali wa shule.