MIAKA 63, BETI 63: Rais wetu Dkt.Samia, sisi twakusalimia

NA LWAGA MWAMBANDE

MHESHIMIWA Dkt.Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja. Ameolewa na Bw. Hafidh Ameir na wamejaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike.

Dkt.Samia ni Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aliapishwa Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye alikuwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dkt.Samia ni mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande licha ya kumtakia heri na mafanikio tele katika siku yake ya kuzaliwa leo, pia amemwandikia beti 63 za shairi. Endelea
;

1. Rais wetu Samia,
Pazuri umefikia,
Duniani kungia,
Sisi twakusalimia.

2.Mungu anakujalia,
Miaka kujipatia,
Neema kwako Samia,
Sisi twakusalimia.

3. Mungu alikupangia,
Duniani kuingia,
Jina lako ni Samia,
Sisi twakusalimia.

4. Aliiandaa njia,
Kwa wazazi kupitia,
Mazoezi yakaingia,
Sisi twakusalimia.

5. Shuleni ukaingia,
Elimu kujipatia,
Ni mbali ulifikia,
Sisi twakusalimia.

6. Shule ni yetu dunia,
Rais umepitia,
Kazini ukaingia,
Sisi twakusalimia.

7. Kazi umetufanyia,
Kwingi ulikopitia,
Nazi twakufagilia,
Sisi twakusalimia.

8. Rais wetu Samia,
Keki utajipatia,
Mwenyewe utajilia,
Sisi twakusalimia.

9. Mungu tunamwangukia,
Azidi kubarikia,
Miaka ya kuzidia,
Sisi twakusalimia.

10. Nafasi washikilia,
Taifa kutumikia,
Pema tuweze fikia,
Sisi twakusalimia.

11. Wakati wafurahia,
Duniani kuingia,
Zidi kutumikia,
Sisi twakusalimia.

12. Mamilioni sikia,
Leo wakufurahia,
Miaka ulofikia,
Sisi twakusalimia.

13. Heri tunakutakia,
Afya njema kuzidia,
Uzidi tutumikia,
Sisi twakusalimia.

14. Rais wa Tanzania,
Tangu ulipoingia,
Mengi tunajivunia,
Sisi twakusalimia.

15. Yale unatufanyia,
Twende mbele Tanzania,
Twaona twaangalia,
Sisi twakusalimia.

16. Yapo yaliyovilia,
Njia metufungulia,
Haya tunafurahia,
Sisi twakusalimia.

17. Yapo ulipoingia,
Tulikuwa twachangia,
Ili kukamilishia,
Sisi twakusalimia.

18. Wapo tulowasikia,
Ya kwamba utafulia,
Malengo hutafikia,
Sisi twakusalimia.

19. Ya Dodoma kuhamia,
Ya kwamba kutafifia,
Tama wanajishikia,
Sisi twakusalimia.

20. Dodoma twafurahia,
Makubwa yafanyikia,
Serikali metulia,
Sisi twakusalimia.

21. Tayari tumesikia,
Msumari pigilia,
Dodoma tushahamia,
Sisi twakusalimia.

22. Miradi inazidia,
Hadhi kupapandishia,
Kilele kukifikia,
Sisi twakusalimia.

23. Hebu Dodoma pitia,
Katalii furahia,
Ya kwangu yataingia,
Sisi twakusalimia.

24. Barabara zazidia,
Miradi twafurahia,
Uwanja wa ndege pia,
Sisi twakusalimia.

25. Eti reli kusinzia,
Kama shimo kutitia,
Yajayo wanasikia?
Sisi twakusalimia.

26. Dar Moro kuingia,
Punde tutafurahia,
Tutakutaja Samia,
Sisi twakufurahia.

27. Kwamba jembe kaishia,
Miradi inaishia,
Tama wanajishikia,
Sisi twakusalimia.

28. Buti umeyavalia,
Tena metuahidia,
Yote utamalizia,
Sisi twakusalimia.

29. Rufiji tumesikia,
Maji tele yaingia,
Umeme twatarajia,
Sisi twakusalimia.

30. Afya tunakimbilia,
Tiba ya kujivunia,
Site tuweze fikia,
Sisi twakusalimia.

31. Wengi wanaangalia,
Kuona na kusikia,
Meno wanajisagia,
Sisi twakusalimia.

32. Vile walifikiria,
Pale utaangukia,
Ndipo unainukia,
Sisi twakusalimia.

33. UVIKO ulikutia,
Wengiwengi twaishia,
Tofauti na dunia,
Sisi twakusalimia.

34. Ukatubadilishia,
Tuliyotumia gia,
Chanjo kwetu kuingia,
Sisi twakusalimia.

35. Wengine walichukia,
Wengine kufurahia,
Tuwe sawa na dunia,
Sisi twakusalimia.

36. Sasa sisi na dunia,
Vema watuangalia,
Hata tukiwafikia,
Sisi twakusalimia.

37. Tulitengwa na dunia,
Yale tulijfanyia,
Huko tulifurahia,
Sisi twakufurahia.

38. Pale ulipoingia,
Mwanga mpya kaingia,
Ikatujua dunia,
Sisi twakusalimia.

39. Leo umri fikia,
Hongera kwako Samia,
Nasi twakushangilia,
Sisi twakusalimia.

40. Mungu wamtumikia,
Kuongoza Tanzania,
Azidi kuangalia,
Sisi twakusalimia.

41. Pale unatamania,
Tanzania kufikia,
Aweze kukujalia,
Sisi twakusalimia.

42. Huku tunashangilia,
Keki tunafurahia,
Siku ya kwako Samia,
Sisi twakusalimia.

43. Miaka twakutakia,
Uzidi kujiishia,
Maisha kifurahia,
Sisi twakusalimia.

44. Mipango mejipangia,
Ya kwako kuifikia,
Uweze kuifikia,
Sisi twakusalimia.

45. Hiyo yako familia,
Waweze kufurahia,
Jinsi wawakumbatia,
Sisi twakusalimia.

46. Hata sisi Tanzania,
Tuzidi kujipatia,
Mema ya kwako Samia,
Sisi twakusalimia.

47. Serikali Tanzania,
Yako Rais Samia,
Uzidi tutumikia,
Sisi twakusalimia.

48. Yale twayachungulia,
Mema ya kujichumia,
Yaweze kutufikia,
Sisi twakusalimia.

49. ARA nne twasikia,
Ambazo wasimamia,
Matunda watupatia,
Sisi twakusalimia.

50. Maridhiano sikia,
Ambayo umekazia,
Wengi wanakusifia,
Sisi twakusalimia.

51. Pale yaliyovilia,
Kisiasa Tanzania,
Unajijenga Samia,
Sisi twakusalimia.

52. Siasa zilizimia,
Huku watu wakilia,
Umeshazifungulia,
Sisi twakusalimia.

53. Mikutano twasikia,
Maneno wanatambia,
Nawe wakushangilia,
Sisi twakusalimia.

54. Katiba wanalilia,
Tamaa kujikatia,
Heri wanapumulia,
Sisi twakusalimia.

55. Haki umekomalia,
Dhuluma kutochangia,
Hili ni hema Samia,
Sisi twakusalimia.

56. Mageuzi watwambia,
Tuzidi yatarajia,
Yako tunafwatilia,
Sisi twakusalimia.

57. Tunaendelea pia,
Kwa kazi kujifanyia,
Kwa maendeleo pia,
Sisi twakusalimia.

58. Ni mvumilivu pia,
Mengi unayasikia,
Bila kukasirikia,
Sisi twakusalimia.

59. Lakini tunasikia,
Ukali wako Samia,
Maamuzi yachangia,
Sisi twakusalimia.

60. Wale wanajifanyia,
Kazi za Watanzania,
Huachi wakatulia,
Sisi twakusalimia.

61. Wazembe kwako walia,
Mbali wawatumbulia,
Wema wazidi nukia,
Sisi twakusalimia.

62. Heri ya kwako Samia,
Miaka kuifikia,
Mola zidi barikia,
Sisi twakusalimia.

63. Sitina tatu Samia,
Miaka imetimia,
Heri tunakutakia,
Sisi twakusalimia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
27/1/2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news