NA ADELADIUS MAKWEGA
JAPOKUWA mirabaha na haki ya wimbo huu zinaelekezwa mno kwa Fadhili William, huku kumekuwa wasanii kadhaa wakidai kuwa wao ndiyo walioutunga wimbo huu maarufu wa Malaika. Wimbo huu kwa miaka zaidi 80 ukiaminika kuwa ulitungwa na kurekodiwa katika mataifa ya Kenya na Tanzania huku ukiwa ni wimbo pekee wenye sumaku kali ya kuitambulisha Afrika ya Mashariki na lugha ya kiswahili.
Malaika ni wimbo unaozungumzia maudhui ya mapenzi ambapo kijana mmoja mdogo anashindwa kumuoa binti mmoja mrembo kwa kuwa hana mali.
Kama waswahili wasemavyo mkono mtupu haulambwi shekhe! Kwa miaka hiyo 80 wimbo huu umeweza kurekodiwa katika matoleo mbalimbali na wanamuziki wa kila aina, kwani nguvu hiyo ya usumaku ya kupendwa karibu mataifa mengi imekuwa bado ikiendelea kuwavutia wasanii wengi na wapenzi na wanamuziki wengi dunia kuurudia kila uchao.
Kutokana na umaarufu wa wimbo huu neno malaika sasa limekuwa pia neno lenye maana nyingi; Kiumbe wa kiroho anayekuwa na umbo la kibinadamu, mjumbe wa Mungu, mlinzi wa binadamu asiyeonekana, mtoto mchanga, pia ni wingi wa neno laika, mwisho ni MWANAMKE MPOLE, MNYENYEKEVU, MWENYE UMBO & SURA NZURI.
Maana hii ya mwisho ya neno LAIKA/MALAIKA ya MWANAMKE MPOLE, MNYENYEKEVU, MWENYE UMBO & SURA NZURI ndiyo iliyokuja baada ya kutumiwa katika wimbo huo kwa miaka zaidi ya 80 katika lugha ya Kiswahili mwanakwetu upo?
Fadhili William ambaye alikuwa mwanamuziki wa Kenya anahusishwa na wimbo huo kutokana na yeye kuwa mtu wa kwanza wa kuurekodi wimbo huo studio na kusaidia kufahamika zaidi na kuchezwa katika kumbi za muziki na redio nyingi Afrika ya Mashariki.
Ndugu William kila mara alikuwa akisisitiza kuwa wimbo huo ni wake huku akieleza namna alivyoweza kuutunga hadi kuurekodi mwaka 1960 na bendi yake ya Jambo Boys. William ambaye ni ni Mkenya huku akiungwa mkono na Wakenya wengi kuwa ndiye mwenye haki na wimbo huo alizaliwa Novemba 11, 1938 kama Fadhili William Mdawida na aliwahi kusimulia namna alivyotunga kibao hicho.
“Nilikuwa na mpenzi wangu aliyekuwa mrembo sana akifahamika kama Fanny na kwa urembo wake nilimpa jina Malaika lakini ilipofika wakati wa kumchumbia binti huyo, nilikosa pesa za mahari kwa kuwa nilikuwa fukara mno, huku baba yangu alifariki wakati nikiwa na miaka miwili tu.
"Umasikini wetu ulifanya Fanny akaolewa na jamaa mwingine tajiri. Ili kupoza maumivu hayo nilimtungia wimbo huu huku mumewe Fanny akiusikiliza katika redio bila ya kujua maana ya fumbo hilo, kumbe malaika ndiye mkewe na mchumba wangu wa zamani.”Hayo ni ya Fadhili William.
Ninapogubua kiganja changu na kuigubika tena shilingi, nagubua na kukutana na upande wa pili wa walio wengi wanaomtaja ndugu Adam Salim kuwa ndiyo mmiliki halali wa wimbo huo. Adam Salim ambaye ni mwandishi wa wimbo huu alizaliwa mwaka 1916 huko Kilimanjaro Tanzania na alitunga wimbo huo mwaka 1945 akiwa Nairobi Kenya.
Katika simulizi za mapenzi wako wanaohonga magari, nyumba, pesa, almasi, dhahabu na kadhalika yote hayo ni kuonesha tu mapenzi kwa yule unayempenda. Kumbuka kila anayehonga hutoa kulingana na uwezo wake. Usimcheke anayehonga simu.
Viatu na kadhalika kumbuka kuwa huo ndiyo uwezo wake. Naye ndugu yetu Adam Salim ambaye alikuwa na mpenzi wake anayefahamika kama Halima Ramadhani Binti Maruwa alimpenda mno huku akitaka kufunga naye pingu za maisha.
Kwa kuwa Adam Salim alikuwa hana pesa Bi Halima alimuacha ndugu Salim na kulipeleka penzi kwa bwana tajiri mwenye asili ya Asia na kufunga naye ndoa mwaka 1945 huko Nairobi.
“Mimi nilikuwa fundi makenika Nairobi Kenya, nikitengeneza magari kadhaa lakini mara baada ya kazi, nikifanya muziki katika kumbi kadhaa za starehe kati ya mwaka 1940-1950, katika kipindi hicho ndipo nilipoutunga wimbo huo kwa Binti Maruwa angalau kupoza moyo wangu baada ya kukimbiwa na mrembo huyu. Fadhili William alikuwa ni miongoni mwa vijana wa rika langu wakati huo ambaye wakati naimba aliusikiliza, akaupenda na kwa bahati mbaya akaurekodi.”
Kwa maelezo hayo ya Adam Salim, alimpoteza mrembo wake Halima Binti Maruwa na kupoteza wimbo wake wa Malaika. Ndiyo kusema Adam Salim aliwapoteza Malaika wawili kwa mpigo.
Kukiwa na madai kuwa Fadhili William alimlipa Adam Salim kiasi cha shilingi 60 za Kenya kama malipo kwa wimbo huo kama shukurani. Huku ikiaminika kuwa pengine Adam Salim na Fadhili William walikuwa na makubaliano ya mdomo baina yao.
Mwanakwetu mimi na wewe hatukuwepo na siri ya mtungi aijuaye ni kata.Huku kukiwa na taarifa chache mno zinazomtaja Adam Salim lakini mwaka 1956 Adam Salim alipata ajali na kulazwa katika hospitali moja Nairobi Kenya na kulala na kuamka wodini kwa miaka mitatu. Alirudishwa kwao Moshi ambapo wazazi wake walikuwa wakiishi huko.
Fadhili William alikwenda mbali na mwaka 1960 aliurekodi wimbo huu akiwa na Jambo Boys Band rasmi kama kibao chake katika studio inayofahamika kama Columba East African Music Company huku akiimba mashairi mawili ya kibao hicho. Naye Adam Salim alipofika Kilimanjaro alienda Morogoro na kuoana na mwanamke mwingine akijipatia riziki yake kwa ufundi wa baiskeli.
Safari ya wimbo huu wenye utata mwingi haikuishia hapo, Miriam Makeba aliichachusha zaidi. Miriam Makeba aliyezaliwa mwaka 1932 na kufariki 2008. Inadaiwa kuwa Makeba alikutana na wimbo huo mwaka 1963 ambapo alitakiwa kuimba katika siku ya uhuru wa Kenya. Akiwa na Hary Belafonte ambaye alikuwa mumewe baadaye.
Mwaka 1963 wakiwa Kenya inadaiwa kuwa huku akisaidiwa baadhi ya maneno ya Kiswahili na Daudi Amunga ambaye alikuwa mwanamuziki mkongwe wa Kenya waliweka nakishi ya wimbo huo kabla kuimbwa kwenye tukio hilo. Huku ikidaiwa kuwa mwanasiasa Tomo Mboya ndiye aliyemsaidia Miriam Makeba kuongeza ubeti wa tatu wenye maneno pesa zasumbua roho wangu.
Fadhili William aliurekodi tena mara baaada ya Makeba kuuweka ubeti wa tatu wenye maneno ya pesa zasumbua roho yangu kama alivyokuwa akiimba Adam Salim katika kumbi za Nairobi Kenya kabla ya kurudi Tanzania.
Miriam Makeba alipokwenda Marekani aliurekodi wimbo huo ikidaiwa kuwa bila ya kibali cha mtu yoyote yule. Jambo hili lilimkwaza Fadhili William na kumpeleka mahakamani Miriam Makeba.
Kumbuka tu ndugu yetu Adam Salim yeye sasa hakuwepo katika ulimwengu wa muziki tena bali alikuwa katika ulimwengu wa ufundi wa baiskeli, peengine akizungukwa na miio ya nyundo ya kuweka spoki, pedeli na madigadi vizuri na kuziba pancha za baiskeli za Waluguru, Wakagauru na Wapogoro hapo Morogoro.
Fadhili William alifanya hivyo akisaidiwa na Mmarekani Peter Colmore na mtayarishaji muziki Charles Worrod. Fadhili William alimshinda Makeba na jambo hilo lilimkwaza mno Miriam Makeba.
Inasadikiwa kuwa Miriam Makeba alikwenda mbali kuendelea kuuimba wimbo huo kila mara na kuingiza maneno kuwa wimbo huu unatoka Tanzania. Hilo lilifanyika katika majukwa kadhaa kila alipopanda na kuimba, katika kila santuri aliyourekodi na kila studio iwe ya runinga au redio iliyochezwa kibao hicho.
Swali la kujiuliza, Je ni kweli Miriam Makeba aliufahamu wimbo huo Kenya mwaka 1963? Kulijibu swali hilo naliweka ubaoni kwako msomaji wa matini zangu.
Lakini kuna jambo nalikumbuka kidogo, kati ya mwaka 2009-2011 nikiwa Mtumishi wa TBC nilipewa kazi kusikiliza rola tatu za sauti na Mtayarishaji Vipindi mwanadamizi wakati huo marehemu Abisai Stephern, moja ya ujio wa Bibi Indira Ghandi nchini Tanzania (1980s), ya pili ilikuwa ni siku ya uhuru wa Tanganyika (1961) na ya tatu ilikuwa siku ya Muungano(1964).
Katika rola moja ya sauti kati ya hizo mbili za mwisho katika dhifa iliyofanyika ikulu ya Tanganyika Miriam Makeba aliimba wimbo wa Malaika, nakumbuka hata MC wa dhifa hiyo iliyofanyika Ikulu alikuwa kama sijakosea ni Mtangazaji wa Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) ndugu Marehemu Godfrey Mgodo.
Binafsi nadhani Miriam Makeba aliufahamu wimbo huo kabla ya 1963.Mgogoro huu wa wimbo Malaika unalinganishwa na wimbo Imbube katika he lion Sleep Tonight wa Linda ambaye hadi anafariki hakuweza kutambulika kuwa ndiye mtunzi wa wimbo huo.
Hata kwa Fadhili William na Adam Salim wamefariki kitambo na hawapo lakini bado swali hilo limekosa wa kulitegua.
Lakini mimi binafsi nina amini kuwa Fadhili William ndiye wa kwanza kuurekodi na kuutangaza mno wimbo huo, huku Adam Salim ndiye aliyeutunga. Ndiyo Kusema Mtanzania aliutunga na Mkenya aliurekodi, kama mirabaha basi tugawane sawa kwa sawa. Je wewe mwanakwetu unasemaje?. Miongoni mwa wanamuziki wengine waliourudia wimbo huo Angeloko Kidjo, Peter Seeger, The Hep Stars, Safari Sound Band, Nana Mouskoum na Boney M.
Huku Bollywood nayo haikuachwa salama na uchawi wa wimbo huu kwani iliutumia katika filamu kadhaa za Kihindi kama wimbo wa kuzisindikiza Tu Jahan Bh Jayeqi na Gawah Hain Chand Taare Gawah Hai.
0717649257