MUKI:Walivyokuchuna wao, kwa sasa hutamaniki

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, watu wengi hufikiri kwamba mwenye fedha nyingi kwa maana ya Muki huwa anazipata tu kwa kuota ndoto ya siku moja.

Mawazo haya, kama umeyaweka katika ufahamu wako, yafaa uyaondoe. Zingatia kwamba wengi wenye fedha nyingi wanazipata kwa njia nyingi, kubwa ikiwa ni kuwekeza.

Kwani, watu wanaamua kufanya biashara endelevu ambazo zimekuwa zikiwaimngizia vipato kila siku, mara nyingi wengi wanafanya kazi sana ili kupata fedha, vivyo hivyo wanajitahidi kadri iwezekanavyo kutunza fedha zao katika mifumo rasmi ikiwemo benki ambapo ni eneo salama la kulinda rasilimali fedha zao.

Wachumi wengi wanasisitiza kuwa,kuwekeza si chanzo cha kukufanya ushinde unafanya starehe au kutumia fedha ovyo badala yake ni kubuni miradi zaidi itakayotunisha mapato yako, jamii uliyoipa ajira na Taifa kwa ujumla.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ukiwa Muki kwa maana ya mtu mwenye fedha nyingi, utapendwa sana na watu, lakini unapaswa kuhakikisha umakini unatawala ili uweze kutumia fedha hizo kuwekeza kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla. Endelea;


1.Wapendwa na watu wengi, sababu wewe ni muki,
Wafurika kwako wengi, wajipatie riziki,
Baraka zako za wengi, wala usiwataliki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

2.Watu wana shida zao, wakitafuta riziki,
Sababu juhudi zao, hawaziondoi dhiki,
Kwako wafanya makao, una mizinga ya nyuki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

3.Wahenga na ngeli zao, semi wamezihakiki,
Kwamba wale wapendwao, ni pesa si urafiki,
Sababu ya mali zao, sababu wao ni muki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

4. Ni wengi na roho zao, waja kwako wewe muki,
Kwako kutabaki kwao, jinsi wabakia muki,
Mali zikienda kwao, kwa hao hufahamiki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

5. Watatoka haohao, hadhara kukudhihaki,
Walivyokuchuna wao, kwa sasa hutamaniki,
Kisha watakwenda zao, ndiyo wamekutaliki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

6. Vuna ya kwako mazao, tajirijika uwe muki,
Ujiwekee mafao, mali uzidi miliki,
Dunia siyo makao, Mola zidi mbariki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

7. Wako wahitaji hao, moyo wako uafiki,
Na wajanjajanja hao, hata hawaaminiki,
Uzijue nia zao, wasikufilisi muki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

8. Usile maneno yao, kukusifu wewe muki,
Uzijue nia zao, sifa wapate riziki,
Dhamiri yako mkao, kuyafanya yako muki.
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

9. Watu chakarika zao, wajihenga wawa muki,
Changamoto kubwa kwao, kubakia kuwa muki,
Watapanya mali zao, kwa uovu kubariki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

10. Usifanye kama hao, kwa Mungu ni mamluki,
Kwani mwisho wao hao, mali zao hazibaki,
Tulia ucheze bao, usalie wewe muki,
Lakini uwe makini, hakiki wabaki muki.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news