NECTA yafuta matokeo,yafungia vituo huku ikiachana na kuwatangaza wanafunzi bora zikiwemo shule

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne uliofanyika Novemba 14 hadi Desemba Mosi, 2022, Tanzania Bara na Visiwani huku likiwafutia wanafunzi 333 kwa udanganyifu.
Katika matokeo hayo, kati ya watahiniwa 520,558 wenye matokeo 456,975 sawa na asilimia 87.79 wamefaulu kwa kupata madaraja ya kwanza hadi la nne huku ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 0.49 kutoka wa mwaka 2021 ambapo watahiniwa 422,388 sawa na asilimia 87.30 walifaulu.

Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Athumani Amasi ameyatangaza matokeo hayo leo Januari 29, 2023 ambapo amesema kati ya watahiniwa hao mmoja ni wa maarifa (QT) na 332 watahiniwa wa shule za sekondari nchini.

"Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 333 kwa kufanya udanganyifu, kati yao mmoja ni mtahiniwa wa maarifa na 332 ni wa shule," amesema Kaimu Katibu Mtendaji huyo.

Amasi ametaja watahiniwa wengine waliofutiwa matokeo ni wanne ambao wameandika matusi katika mitihani yao ambapo pia vituo vitatu vimefungiwa kufanya mitihani baada ya kuthibitika kupanga na kufanya udanganyifu.

Kaimu Katibu Mtendaji huyo amevitaja vituo hivyo kuwa ni Andrew Faza Memorial cha Kinondoni jijini Dar es Salaam, Cornelius cha Kinondoni na Mnemonic Academy cha Halmashauri ya Mjini Magharibi jijini Zanzibar.

Wakati huo huo NECTA wamesitisha utaratibu wa kutangaza shule bora na mwanafunzi bora wa matokeo ya kidato cha nne.

Amasi amesema, utaratibu huo wa kutangaza shule bora ulikuwa unazitangazia biashara baadhi ya shule nchini.

"Kutangaza shule ya kwanza huenda tulikuwa tunakufanyia marketing (masoko) kwa kuitaja tu hiyo shule, shule zipo nyingi zaidi ya elfu 18, sasa unapotaja moja sidhani kama ina tija,"amesema Kaimu Katibu Mtendaji huyo.

Haya hapa Matokeo ya Kidato cha Nne 2022

Aidha, kuhusu kumtangaza mwanafunzi bora wa mtihani huo amesema hakuna tija katika hilo kwani hauwezi kumtangaza mwanafunzi mmoja katika ya wanafunzi wote Tanzania ambao huenda pia mazingira yao ya kusoma yalikuwa tofauti.

"Unamtaja mtu kwamba ameongoza katika kundi ambalo pamoja na kwamba wamefanya mtihani huo huo lakini hawakusoma katika mazingira yanayofanana, halafu sasa unampa sifa mtu mmoja,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news