NA DIRAMAKINI
BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili kwa wanafunzi waliofanya mtihani mwaka 2022.
Akitangaza matokeo hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Athumani Amasi amesema, ufaulu umeshuka ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo kwa darasa la nne ufaulu ni asilimia 82.95 ikilinganishwa na asilimia 86.30 mwaka 2021.
Darasa la Nne, jumla ya wanafunzi 1,320,700 kati ya 1,592,235 wenye matokeo sawa na asilimia 82.95 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B, C na D.
Kwa mujibu wa Kaimu Mtendaji wa NECTA, Athumani Amasi, kati ya wanafunzi waliofaulu wasichana ni 694,547 sawa na asilimia 84.76 na wavulana ni 626,153 sawa na asilimia 81.03.
Kwa upande wa kidato cha pili ufaulu ni asilimia 85.18 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 92.32.
Aidha, NECTA imezuia matokeo ya wanafunzi 442 wa darasa la nne na wanafunzi 258 wa kidato cha pili waliopata matatizo ya afya na kushindwa kukamilisha mtihani wa upimaji wa kitaifa.
"Mwaka 2021 wanafunzi waliofaulu walikuwa 1,347,554 sawa na asilimia 86.30,” amesema Amasi.
Wakati ufaulu ukishuka, somo la Kiingereza limeendelea kuwa changamoto kwa wanafunzi baada ya asilimia 79.89 ya watahiniwa wote wa Darasa la Nne kupata daraja D na E.
Pia, asilimia 82.09 ya watahiniwa wote walipata daraja D na E katika somo la Hisabati.
NECTA pia, imefuta matokeo ya wanafunzi 213 wa darasa la nne na wanafunzi 52 wa kidato cha pili ambao walibainika kufanya udanganyifu.
Pia,NECTA imefungia vituo viwili kati ya vituo 18,645 vya mitihani vilivyothibitika kupanga na kufanya udanganyifu.
Wakati huo huo, NECTA imesema wanafunzi 2,095 kati ya 2,180 waliofanya mtihani wa marudio wa darasa la saba uliofanyika kati ya Desemba 21 na 22,2022 wamefaulu daraja A hadi C sawa na asilimia 96.1.
Wanafunzi hao ni kati ya 2,194 waliofutiwa matokeo ya mtihani huo na NECTA baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu uliofanyika Oktoba 5, 6 mwaka 2022.
Amasi amesema, kati ya wanafunzi 2,194 waliofutiwa matokeo waliofanya mtihani 2,180, wachache hawakushiriki mchakato huo kwa sababu mbalimbali, akisema huenda wengine walikwenda nje ya nchi kujiendeleza.