NA LWAGA MWAMBANDE
DESEMBA 31, 2022 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi alifuta sherehe za Mapinduzi na kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hizo za miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu iliyokuwa zifanyike Januari 12, 2023 zitumike katika sekta ya elimu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwiyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla (kulia) na viongozi wengine wakipata maelezo kutoka kwa mwanafunzi Khalfani Abdalla Saidi wakati alipotembelea katika chumba cha Somo la Sayansi wakati alipoifungua rasmi Skuli mpya ya Sekondari ya Salum Turky kwa-Binti Amran jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Rais Dkt.Mwinyi katika mkutano na vyombo vya habari Ikulu jijini Zanzibar alisema awali sherehe za Mapinduzi Matukufu zilipangwa kutumia shilingi milioni 700 licha ya gharama kupunguzwa hadi kufikia shilingi milioni 450, ambazo amesema serikali imezielekeza kuongeza nguvu kwenye sekta ya elimu ikiwemo madarasa, madawati, maabara na huduma nyingine za elimu.
Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hufanyika kila mwaka Januari 12. Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yalitokea mwaka 1964 kwa kumuondoa madarakani Sultani wa Zanzibar. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, hilo ni jambo la heri huku akisisitiza miaka 59 ni mingi ya kumshukuru Mungu, kwani huo ni umri wa mtu mzima. Endelea;

1.Umri mtu mzima, haya yetu Mapinduzi,
Watoto watu wazima, na sasa ni viongozi,
Tunazidi kujituma, kuyaenzi Mapinduzi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
2.Zanzibar metoka mbali, inazidi panda ngazi,
Kwa matendo na kauli, ni kuenzi Mapinduzi,
Kwa wote ya kibali, na kizazi hata kizazi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
3.Waliinuka wazazi, wakafanya Mapinduzi,
Kuwatoa walowezi, walioringia ngozi,
Ilikuwa ngumu kazi, ilohitaji ujuzi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
4.Karume Mzee wetu, liongoza Mapinduzi,
Wengine wazee wetu, lishiriki Mapinduzi,
Kwa haya maisha yetu, yachangia Mapinduzi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
5.Muungano niutaje, linogesha Mapinduzi,
Viongozi niwataje, waliufanyia kazi,
Karume na Nyerere je, walilinda Mapinduzi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
6.Akaja Aboud Jumbe, alilinda Mapinduzi,
Hivi ni nani atambe, ayumbishe Mapinduzi,
Haruhusiwi mzembe, kuchezea Mapinduzi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
7.Na Ali Hassan Mwinyi, alilinda Mapinduzi,
Ni Uhuru si umwinyi, unaofanyiwa kazi,
Fujo watu hawafanyi, kuchezea Mapinduzi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
8.Na Idris Wakil, Baraza la Mapinduzi,
Aliongoza kamili, rais mfanyakazi,
Akafikisha mahali, kuikamilisha dozi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
9.Vyama vingi kuingia, kwa kweli likuwa kazi,
Salmin kuingia, alilinda Mapinduzi,
Amani Karume pia, kweli alifanya kazi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
10.Kuja Dokta Shein, alijitangaza wazi,
Ya kwamba yuko kazini, kuyaenzi Mapinduzi,
Alivyokuwa makini, alifanya nyingi kazi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
11.Dokta Mwinyi tunaye, Baraza la Mapinduzi,
Mwenyekiti huyu naye, anafanya vema kazi,
Maendeleo ni yeye, analeta mapinduzi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
12.Nchi inasonga mbele, kuyaenzi Mapinduzi,
Uchumi Buluu tele, ndio wafanyiwa kazi,
Wanacheza kama Pele, jinsi inakwenda kazi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
13.Heri tunawatakia, Baraza la Mapinduzi,
Kuzidi yasimamia, matukufu Mapinduzi,
Zanzibar ya Tanzania, izidi kupanda ngazi,
Hamsina tisa myaka, ni shangwe za Mapinduzi.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602