Ni wanafunzi 4,224 tu ndio waliochaguliwa kwenda Kidato cha Kwanza 2023 shule za bweni, kwa nini?

NA OR-TAMISEMI

SIKU za hivi karibu kumezuka taharuki kwa wananchi wengi, wakihoji namna ambavyo wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza hususani wale wa shule za bweni walivyochaguliwa.

Ni wazi kila mzazi anatamani mtoto wake achaguliwe katika shule hizi za bweni,lakini kiuhalisia haiwezekani na waliochaguliwa ni wale tu waliokidhi vigezo.
Kutokana na hali hiyo,Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- TAMISEMI anayesimamia Elimu, Dkt. Charles Msonde mwishoni mwa mwaka alifanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kukagua ujenzi wa miundombinu ya madarasa yatakayopokea wanafunzi wa kidato cha kwanza,2023.

Akiwa katika ziara hiyo,Dkt.Msonde alitumia wasaa huo kutoa ufafanuzi wa namna ambavyo uchaguzi wa wanafunzi wa shule za bweni umefanyika.

Dkt.Msonde alisema, idadi ya wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 ni 1,073,941 na kati ya hao waliochaguliwa kujiunga na shule za bweni ni 4,224 tu, utaona idadi hii ni sawa na asilimia 0.39 ya wanafunzi wote waliochaguliwa.

Kwa nini idadi ni ndogo ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za bweni?.

Dkt. Msonde anafafanua kuwa, idadi ya shule za Sekondari za Serikali zinazochukua wanafunzi wa kidato cha kwanza ni 4,307 na kati ya hizo shule za Sekondari za kutwa ni 4,269 na shule za Sekondari za Serikali zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wa bweni wa kidato cha kwanza ni 38 tu.

Anaendelea kufafanua kuwa,kutokana na idadi hiyo ya shule za bweni tulizonazo ili watoto waweze kukaa darasani vizuri, kulala bwenini kwa mujibu wa muongozo, shule hizo 38 zina uwezo wa kupokea wanafunzi 4,224.

Wanafunzi wa bweni walipatikanaje?

Aliendelea kufafanua kuwa,uchaguzi wa wanafunzi wa kwenda bweni kwanza umezingatia viwango vya ufaulu hivyo wale wenye viwango vya juu sana ndio waliochaguliwa. Lakini,hata hivyo waliofaulu kwa viwango vya juu pia ni wengi, hivyo mfumo ulitumika kuchagua wale waliofauli zaidi ya wenzao.

“Hapa tunasema waliochaguliwa kwenda bweni wamepata daraja la kwanza (A), lakini ukiangalia waliopata daraja hilo wapo wanafunzi 50,475, hivyo hata kwenye daraja hili la kwanza ipo kanuni iliyotumika ya kugawa nafasi za wanafunzi waliofaulu vizuri."

Ifahamike kuwa, shule za bweni zimegawanyika katika makundi matatu; Kundi la kwanza ni lile lenye ufaulu wa juu, kundi la pili ni Shule za bweni ufundi na kundi la tatu ni shule za bweni kawaida.

Aliendelea kufafanua kuwa, shule zenye ufaulu wa juu ziko saba tu na zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 932 ambao ndio waliopangiwa huko, kisha shule za bweni ufundi ambazo ziko tisa zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,323 kna Bweni kawaida zimechukua wanafunzi 1,816 na bweni umiliki wa mkoa 153.

Dkt. Msonde alibainisha kuwa, shule hizo za bweni ni za Kitaifa, hivyo uchaguzi wa wanafunzi wa kwenda katika shule hizo pia unafanyika kitaifa kwa maana kuwa kila mkoa na halmashauri nchini lazima zitoe wanafunzi watakaokwenda kusoma katika shule hizo.

Hapa tunaona wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja kwanza (A) wako 50,475 na kati ya hao waliochaguliwa ni 4,224, hivyo kwenye shule za bweni zenye ufaulu wa juu tunatumia uwiano wa idadi wa watahiniwa katika Mkoa A mara Idadi ya nafasi zote kwa watahiniwa waliofaulu zaidi gawanya kwa jumla ya watahiniwa wote kitaifa hapo utapata idadi ya nafasi za bweni kwa watahiniwa waliofaulu zaidi kwenye Mkoa A.

Kanuni hiyo hiyo itatumika kwenye Mkoa kupata idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kwenda kwenye shule zenye ufaulu wa juu kutoka Mkoa husika.

Kanuni hii pia itatumika kupata wanafunzi waliochaguliwa kwenye shule za bweni za ufundi kutoka kwenye Mikoa yote nchini.

Kwa upande wa shule za bweni kawaida kanuni yake ni uwiano wa watahiniwa wote wa darasa la VII katika shule za vijijini/mazingira magumu katika Halmashauri A mara iidadi ya nafasi zote za bweni kwa wavulana na wasichana wa kidato cha kwanza wa vijijini/mazingira magumu Tanzania baraba gawanya na idadi ya watahiniwa wote wa darasa la VII katika shule za vijijini/mazingira magumu Tanzania bara hapo utapata nafasi za bweni za kidato cha kwanza kwa Halmashauri A.

Ikumbukwe kuwa nafasi hizi ni kwa wanafunzi wote waliosoma shule za Serikali na Binafsi katika Mkoa na Halmashauri husika.

Kwa shule za kutwa jumla ya wanafunzi 1,069,717 walichaguliwa kwenda kwenye shule hizo ambapo kila wanafunzi aliyefaulu na kukosa nafasi kwenye ushindani wa shule za Bweni alipangiwa kwenye shule ya Sekondari ya kutwa iliyokaribu (Catment schools) na shule ya msingi aliyosomea.

Dkt. Msonde alihitimisha kuwa sambamba na kanuni zilizotumika na muongozo wa uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mfumo ndio uliotumika kufanya chaguzi hizo hii kupunguza changamoto za kibanaadamu ambazo zingeweza kuleta mgongano wa kimaslahi.

“Kila mwanafunzi aliyechaguliwa kwenda shule ya bweni anakidhi vigezo vyote hata ukiingia kwenye mfumo utaona kuwa vigezo vyake ni vya juu kuliko wengine waliokwenda kwenye shule za kutwa katika hili watoto wa Taifa hili kutoka pembe zote za nchi wenye vigezo wamechaguliwa kwenda kwenye shule za bweni ili kuleta utaifa na umoja kwa watoto wetu.

"Niweke wazi kuwa ufaulu wa daraja la kwanza yaani A unaanzia kwenye maksi 241-300 sasa wazazi/walezi wengi wanaona gredi,lakini sisi tunaoingia kwenye mfumo tunaona alama sasa mtaona kwamba takribani wanafunzi 46,251 wenye ufaulu wa daraja la kwanza (A) wamepengiwa kwenye shule za kutwa kutokana na uhaba wa nafasi za bweni.

"Lakini wale waliopangiwa bweni wanaufaulu wa daraja la kwanza wa maksi za juu zaidi kuliko wale 46,251; Na ndio maana tulivyofika ukomo wa idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kwenda bweni wale waliobakia wenye ufaulu wa daraja la kwanza wote waliopangiwa kwenye shule za kutwa,"amefafanua.

Pia, Dkt.Msonde aliwasihi wazazi kuhakikisha wanafunzi wote waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza, 2023 wanaripoti shule kwa wakati ili waweze kuanza masomo kwa awamu moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news