Nimeridhika na hatua hii-Mhandisi Sanga

NA MOHAMED SAIF

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi wa shilingi Bilioni 24.6 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka kwenye Miji ya Tinde mkoani Shinyanga na Shelui mkoani Singida.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akiwa katika Tenki la Maji wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa kutoa Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Tinde na Shelui.

Mhandisi Sanga amedhihirisha hayo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kukagua utekelezwaji wa mradi kwenye miji hiyo Januari 4, 2023.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha fedha za utekelezaji wa miradi ya majisafi na salama zinapatikana kwa wakati na hivyo kuwawezesha wakandarasi kutekeleza miradi hiyo kwa mujibu wa mikataba yao.
Muonekano wa Tenki la maji Tinde lililojengwa kupitia Mradi wa kutoa Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Tinde na Shelui.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha fedha za utekelezaji wa mradi huu zinapatikana kwa ajili ya wananchi wa Tinde na Shelui,”amesema Mhandisi Sanga.

Akizungumzia hali ya utekelezaji wa mradi kwa ujumla wake baada ya ziara yake kwenye miji yote miwili, Mhandisi Sanga amebainisha kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi imekamilika kwa asilimia 99 kwa maeneo yote mawili kwani tayari maji yamefika kwenye matenki.

Amesema hatua inayofuata ni ujenzi wa mtandao wa kilomita 32 wa kusambaza maji kwenye miji yote miwili huku kila mji ukijengewa kilomita 16 za mtandao.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akisisitiza jambo wakati wa ziara yake kwenye Mradi wa kutoa Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Tinde na Shelui. Kulia ni Mtaalam Mshauri kutoka Kampuni ya WAPCOS Ltd, Arnab Saha.

Hata hivyo, amebainisha kwamba kwa upande wa Shelui tayari wananchi wameanza kutumia maji kutoka Ziwa Victoria kwakuwa wameunganisha kwenye mfumo wa usambazaji uliokuwepo tangu zamani na kwamba kinachofuata kwa Mji wa Tinde ni kuhakikisha maji yanasambazwa kwa watumiaji.

“Nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa, ninampongeza Mkandarasi Kampuni ya Megha Engineering and Infrastructure Ltd pamoja na Mtaalam Mshauri Kampuni ya WAPCOS Ltd kwa kukamilisha mradi huu,” amesema Mhandisi Sanga.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akijadiliana jambo na watendaji wanaosimamia Mradi wa kutoa Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Tinde na Shelui.

Amefafanua kwamba mradi wa kupeleka maji kwenye miji ya Tinde na Shelui unatoa maji kutoka katika mradi mkubwa wa Kahama-Shinyanga ambao pia umepeleka maji kwenye Miji ya Tabora, Igunga na Nzega.

Aidha, Mhandisi Sanga amewapongeza wasimamizi wa mradi ambao ni Mamlaka za Maji za Shinyanga na Igunga kwa kushirikiana na Jumuiya za Watumia Maji Shelui pamoja na watendaji wa Wizara ya Maji wanaosimamia mradi huo moja kwa moja.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akiwa Tinde kwenye eneo la Mradi wa kutoa Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Tinde na Shelui.

Vilevile amewasihi watumishi wa Wizara ya Maji na Mamlaka za maji kuhakikisha miundombinu inalindwa na pia mazingira yanatunzwa ili kuwa na mradi endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news