NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa miundombini katika Shule ya Sekondari mpya ya Bwai iliyopo katika Kata ya Kiriba wilayani humo.

Sekondari hii ilifunguliwa wiki iliyopita na hadi jana Januari 19, 2023 wanafunzi 125 kati ya 153 tayari wameanza masomo yao ya Kidato cha Kwanza (Form I) sawa na asilimia 77.85 wameanza masomo.

Harambee hiyo inalenga ukamilishaji wa vyumba vitatu vya madarasa. Kwa sasa, vyumba vilivyokamilika na vinatumika ni vitatu. Ujenzi wa choo kipya chenye matundu manne. Kwa sasa, ipo choo chenye matundu nane.

Aidha, ujenzi ni endelevu, na michango ni endelevu hadi hapo miundombinu muhimu itakapokamilika, ikiwemo, maabara tatu za masomo ya sayansi, maktaba, nyumba za walimu, viwanja vya michezo.

Mbunge wa jimbo, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo amechangia saruji mifuko 100, mabati bando mbili (mabati 24).

"Wanakijiji wakiwemo wazazi wa wanafunzi wanaosoma hapo, wameamua kuajiri walimu wa kujitolea kwa posho ya shilingi 200,000 kwa kila mwalimu kwa mwezi. Wazazi watachangia Shilingi elfu 3,000 kila mwezi."imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Mbunge wa jimbo, Prof. Muhongo atachagia shilingi 100,000 kwa kila mwalimu kwa mwezi, yaani jumla ya shilingi 300,000 (laki tatu) kila mwezi kwa walimu watatu.