NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo anatarajia kufanya kikao na wakuu wa shule zote za sekondari jimboni humo.
Hayo yamebainishwa Januari 11, 2022 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo."Jimbo la Musoma Vijijini lenye kata 21 lina jumla ya sekondari 27 ambazo 25 ni za kata kwa maana ya Serikali na mbili ni za madhehebu ya Dini SDA na Katoliki,"imeeleza taarifa hiyo.
"Mbunge wa Jimbo ataitisha kikao cha kutathmini matokeo ya mitihani ya Kidato cha Pili (Form II) na Kidato cha Nne (Form IV."
Ambapo lengo kuu la kikao hicho ni kutathmini matokeo ya mitihani ya vidato hivyo viwili kwa wanafunzi wa Musoma Vijijini. Kutoa mapendekezo ya kuboresha mbinu za kujifunza (uelewa) na kufundisha.
"Mahali pa kufanyika kikao ni Busambara Sekondari tarehe ya kikao itategemea upatikanaji wa Matokeo ya Mitihani ya Form IV 2022. Usafiri na chakula, Mbunge wa jimbo atagharamia."imeeleza taarifa hiyo na kuongeza kuwa.
Miaka kadhaa ya nyuma, Mbunge huyo alishirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mara kufadhili Kongamano la Kuboresha Elimu mkoani Mara. "Hivyo walimu wakuu (Headmasters) wa sekondari zote 27, wanaombwa kujitayarisha."imesema taarifa hiyo.
Said Peter ni mkazi wa Kata ya Etaro katika Jimbo la Musoma Vijijini ambapo amepongeza uamuzi wa mbunge huyo kwa kusema kikao hicho anaamini kitakuwa na tija kubwa katika kuhakikisha sekta ya elimu jimboni humo inazidi kuimarika.
"Prof.Muhongo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha elimu katika Jimbo la Musoma Vijijini inaimarika, tumekuwa tukiona juhudi zake kuhamasisha wananchi kusomesha watoto, kusaidia ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia fedha za mfuko wa jimbo, ushiriki wake katika ujenzi wa madarasa, kusaidia wanafunzi vifaa vya shule na fedha wanaotoka kaya zisizokuwa na uwezo waweze kwenda shule pamoja na kushirikiana na serikali katika miradi ya elimu na miradi mingine hakika Mbunge wetu anachapa kazi sana,"amesema Said Peter.