Rais Dkt.Mwinyi aendelea kuifungua Pemba kiuchumi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema azma yake ya kuifungua Pemba kiuchumi na kuifanya kuwa kituo mahsusi cha uwekezaji sasa inakaribia na kueleza kuwa hatua za utekelezaji wake zimeanza rasmi.
Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Januari 4, 2023 kwenye hafla ya kushuhudia utiaji wa saini wa makubalino ya Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na

Uongozi wa Kampuni ya Propav kutoka Brazil pamoja na Kampuni ya Mecco ya Tanzania, hafla iliyofanyika Ikulu jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji saini wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege Pemba,kati ya Kampuni ya Propav kutoka nchini Brazil pamoja na Kampuni ya MEECO ya Tanzania na Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar , Bi.Khadija Khamis Rajab akisaini kwa niaba ya wizara na Bw. Leondro Motta akisaini kwa niaba ya Kampuni ya Propav ya Brazil,hafla hiyo imeyofanyika Januari 4, 2023 katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Amesema, ni lazima Pemba kuifungua kwa kujengwa miundombinu ya kisasa ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege pamoja na kuimarishwa kwa bandari na ujenzi wa barabara.

Kwa upande wa kuimarisha miundombinu ya bandari, Rais Dkt. Mwinyi amesema, tayari kazi za ujenzi wa Bandari ya Mkoani imeanza na inaendelea vizuri na ujenzi wa Bandari ya Shumba tayari umekabidhiwa kwa mkandarasi wake.

Akizungumzia ujenzi wa barabara kisiwani humo, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza mkataba huo pia utajumuisha ujenzi wa barabara kutoka Chake Chake hadi Mkoani.

Aidha, ameitaka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara kwenye maeneo ya uwekezaji Micheweni, Pemba.

Naye Balozi wa Uingereza nchini, David Concar amesema anaunga mkono juhudi za maendeleo zinayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kwamba Uingereza ni mshiriki wa muda mrefu kwa mataifa mawili hayo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohamed ameeleza mkataba wa ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba utajumuisha awamu mbili tofauti ambapo awamu ya kwanza utajumuisha ujenzi wa jengo la abiria lenye ukubwa wa mita za mraba 9170 pamoja na ujenzi wa njia ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 2510 na upana wa mita 25.

Amesema, katika hatua za awali za ujenzi huo utakamilisha huduma zote muhimu za kuufanya uwanja huo kuwa na hadhi ya kimataifa kwa mujibu wa maelekezo ya Shirika la Kimataifa la Huduma za Usafiri wa Anga Duniani (ICAO). Sambamba na kuruhusu kutua ndege za kimataifa aina ya 737-800 zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 189.

Ameongeza kuwa, hadi kukamilika kwake uwanja utakuwa na uwezo wa kuwahudumia abiria 750,000 kwa mwaka kutoka abiria 45,000 waliokua wakihudumiwa awali.

Ameeleza katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo, utakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 330,000 kwa mwaka ambapo kwa sasa unahudunia zaidi ya abiria laki moja kutoka na ufinyu wa uwanja wa sasa.
Dkt. Khalid ameeleza makataba huo pia utajumisha ujenzi wa kilomita 43 za barabara kutoka Chake Chake - Mkoani, ujenzi wa kilomita 48 za barabara kutoka Fumba - Kisauni na ujenzi wa kilomita 12 za barabara kutoka Tunguu hadi Makunduchi.

Naye mwakilishi wa Kampuni ya Propav ya Brazil, Bw. Leandro Motta amesema, kukamilika kwa ujenzi huo kutaifungua Pemba kijamii na maendeleo kutokana na sera yake ya uchumi wa Buluu kutaimarisha maendeleo na utalii.

Hafla ya utiaji wa saini wa makubalino ya Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Uongozi wa Kampuni ya Propav kutoka Brazil pamoja na Kampuni ya Mecco ya Tanzania ulishuhudiwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Makamu wa Kwanza na Wapili wa Rais Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akibadilishana mawazo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar (katikati) mara baada ya hafla ya utiaji saini makubaliano ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba, baina ya Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar na Kampuni ya Propav kutoka nchini Brazil na Kampuni ya Mecco Tanzania, hafla iliyofanyika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar katika mwendelezo wa shamra shamra za miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, kushoto ni Balozi wa Heshima wa Brazil hapa Zanzibar, Mhe.Abdulsamad Abdulrahim.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Ardhi, Mawasiliano na Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Makatibu na manaibu makatibu wakuu wa serikali ya Zanzibar, Mufti mkuu wa Zanzibar, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wageni wengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news