NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kukamilika kwa diko la kisasa na Soko la Samaki Malindi ni ushuhuda wa vitendo kwa Wazanzibari kutafsiri maana halisi ya Uchumi wa Buluu, visiwani.
Rai wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishiriki katika mnada wa samaki katika Diko na Soko la Samaki Malindi Wilaya ya Mjini Unguja, huku wakinadiwa samaki aina ya Jodari na dalali wa soko hilo, Bw.Ali Hassan Mchoro, samaki huyo ameuzwa kwa shilingi 95,000 Januari 10, 2022. (Picha na Ikulu).
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipofungua diko hilo ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema, Uchumi wa Buluu unakamilishwa na mambo matano muhimu ukiwemo utalii ambao kwa visiwa vya Unguja na Pemba una vivutio vizuri vinavyoingiza wageni kila uchao, uvuvi wa mwani na bahari alisema ni uchumi unaoendelea kufanywa wa wananchi wa visiwa wiwili hivyo, mafuta na gesi pamoja na usafirishaji wa majini na maeneo ya bahari ambayo hutoa fursa nyingi za kiuchumi kwa wakaazi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, wakati Uchumi wa Buluu unagusa zaidi sekta ya uvuvi,kuna haja ya wavuvi kutumia vyombo vya kisasa vya kuvulia zikiwemo zana za utambuzi wa samaki kwenye bahari, zana za GPS ambazo zitaongeza weledi wavuvi, kuvua kiwango kikubwa cha samaki wenye ubora.
Nakuongeza kujengwa vyumba vya kuhifadhia baridi kwa ajili ya kuwekea samaki muda mrefu, mitambo ya kutengeneza barafu pamoja na viwanda vya kuchakata samaki kwa lengo la kuwasafirisha nje ya nchi pamoja na kuwa na babdari ya uvuvi ni mambo ya kuzingatiwa kwenye sekta hiyo.
“Tumeanza kuwawezesha wavuvi wetu kwa vyombo vidogovidogo, nataka tufike katika vile vyombo vikubwa ili wavuvi wetu waje na samaki wakubwa zaidi,”ameeleza Dkt.Mwinyi.
Aidha, ameeleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Nane itawazezesha wavuvi kufikia azima ya Uchumi wa Buluu kwa vitendo na kuongeza kuwa serikali inakusudia kujenga madiko na masoko ya kisasa ya samaki kwa mikoa yote ya Unguja na Pemba.
Hata hivyo, Rais Mwinyi amesema serikali pia itashirikiana na sekta binafsi kuimashirisha mafanikio ya soko hilo na kufahamisha serikali pekee haitoshi kukalisha kila kitu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla amesisitisha suala la usafi na kuziagiza mamlaka husika za diko hilo kusimamia vyema kutunza haiba na mandhari ya eneo hilo.
Naye Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Suleiman Masoud Makame amesema,wizara yake itashirikiana na serikali ya Mkoa wa mjini Magharibi kuhakisha diko na soko hilo yanaendelea kudumu na ubora wake
Mapema akizungumza kwenye hadhara hilyo, Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Yamamura Naofumi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mshirika mzuri na shirika hilo wamekuwa bega kwa bega kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo maji safi, umeme, barabara, afya na elimu.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini, Yasushi Misawa aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kuipa ushirikiano wa kila hali na kueleza kwamba yeye ni muumini mzuri wa masoko ya samaki hivyo, aliwasihi wasimamizi wa diko hilo kuendelea kulitunza ili liishi muda mrefu, aidha, alieleza Tanzania na Japan ni washirika wa muda mrefu na kwamba uhusiano wa pande mbili hizo umejenga historia kubwa baina yao
Diko la Soko la samaki la Malindi limejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) linajumuisha ujenzi wa bandari na diko la maegesho ya boti, jengo jipya la soko na ofisi zake, miundombinu ya kuhifadhia samaki, mtambo wa kuzalisha barafu pamoja na ukarabati wa soko la zamani.
Aidha, diko hilo linatarajia kuhudumia watumiaji 6,500 wakiwemo wavuvi, madalali, wachuuzi, wauzaji rejareja, washushaji wa samaki, wasarifu samaki, walaji na wanachi wengine.
Pia lina maeneo sita ya kuendeshea mnada, meza 141 za wauzaji wadogo wadogo zikiwemo baraza 76 na meza za kuhamishia 65, sehemu 13 za kuparia samaki, ujenzi wa diko la maegesho ya vyombo vidogo vipatavyo 392 kwa siku moja, vyoo 14, sehemu sita za kuogea, vyumba vya kuhifadhia samaki wa tani 200 kwa wakati mmoja pia diko hilo linatarajia kutoa ajira 1,400 kwa ajili ya kushusha na kuhifadhi samaki.
Tags
Habari
Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu Zanzibar
Soko la Samaki Malindi
Uchumi wa Buluu
Ukusanyaji wa Mapato Zanzibar
Zanzibar