NA DIRAMAKINI
MSARIFU wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation (BMF), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameueleza uongozi wa taasisi hiyo kuendelea kuboresha mifumo ya afya kwenye taasisi yao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, ameutaka uongozi huo kuangalia kwa upana jinsi ya kukamilisha miundombinu ya vifaa tiba pamoja na kuimarisha mifumo ya mawasiliano itakayotoa huduma bora kwa walengwa na kuboresha utendaji kwa kuongeza nguvu kazi za ajira ili kutanua wigo kwenye taasisi hiyo.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na uongozi na wafanyakazi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation Ikulu jijini Zanzibar.
Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na taasisi hiyo katika kuimarisha huduma bora za afya pamoja na kupongeza juhudi za BMF katika utendaji kazi wake nchi nzima, Bara na Zanzibar.
Mbali na kusifu jitihada zinazochukuliwa na uongozi kwa kuisimamia vyema taasisi hiyo, pia Dkt. Mwinyi amewataka watendaji na wafanyakazi wa BMF kuanzisha bima ya afya kwa lengo la kwenda sambamba na mahitaji ya wananchi.
Katika hatua nyingine Rais Dkt Mwinyi aliwatunuku vyeti, tuzo na fedha taslimu wafanyakazi waliofanya vizuri kwenye taasisi hiyo kwa kipindi cha utumishi wao pamoja na kuwapongeza.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya BMF, Balozi Tuvako Manongi amesema, bodi yao imeendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali zikiwemo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wadau wa maendeleo wakiwemo wafadhili kutoka sekta za umma na binafsi pamoja na wachangiaji binafsi katika kuhakikisha wanapata rasilimali fedha.
Aidha, alieleza wanaboresha utendaji wa taasisi hiyo kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kupunguza gharama za uendeshaji na kufanyakazi kwa weledi na kuongeza kuwa walifanikiwa kutekeleza miradi mikubwa na midogo kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 ambayo iliboresha huduma za afya kwa mikoa 25 ya Bara na mitano ya Zanzibar, ikiwemo kuongeza rasilimali watu, kuimarisha miundombinu ya majengo na vifaa tiba pamoja na kukabiliana dhidi ya mapambano ya Ukimwi, kifua kikuu na UVIKO 19.
Hata, hivyo ameahidhi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya taasisi hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kufanikisha dira ya taasisi yao.
Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation iliasisiswa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.