NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imejipanga vizuri kuiletea mabadiliko makubwa katika Sekta ya Elimu visiwani humo ili kuongeza ufaulu kwa wanafuzi wengi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya kompyuta mpakato mwanafunsi wa Skuli ya Sekondari ya Lumumba kidato cha nne Msabaha Shaban Kassim, kwa kufanya vizuri mitihani yake ya kidato cha nne mwaka 2022 na kupata Daraja la Kwanza kulia ni Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe.Leila Mohammed Mussa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Tanzania, Mhe. Prof.Adolf Mkenda, hafla hiyo ya kukabidhiwa kompyuta kwa wanafunzi wa kidato cha sita na cha nne waliofanya vizuri mitihani yao kwa mwaka 2022, iliyofanyika Januari 11, 2023 katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Januari 11, 2023 Ikulu mjini Unguja alipowakabidhi kompyuta wanafunzi 1,142 waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha nne na sita ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake kwao.
Ameeleza Serikali ilivyojipanga kuboresha miundombinu kwa kuelendelea kujenga skuli mpya za ghorofa zenye kompyuta, maktaba na maabara kwa msingi na sekondari pamoja na kuondosha mikondo kwenye skuli zote za serikali ili wanafunzi wasome mara moja tu kwa awamu.
“Tuna uhaba wa walimu katika fani mbalimbali hususanI walimu wa sayansi na Hesabati, kwa hiyo lazima tuongeze walimu wa sayansi, lazima tuongeze walimu wa hesabati, lazima tuongeze mafunzo kwa waalimu ili watoe watalamu wengi wa sayansi,” ameeleza Dkt.Mwinyi.
Aidha, amewataka watendaji wa Wizara ya Elimu kurejesha utamaduni wa ukaguzi kwa skuli ya serikali pamoja na kuangalia upya suala la lugha kwa wanafunzi wa madarasa ya msingi ili kuondosha changamoto ya kutojua lugha kwa wanafunzi kwenye skuli za serikali.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Prf.Adolf Mkenda alieleza hatua ya Dkt.Mwinyi kuwazawadia wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa itachochea juhudi za kuongeza ufaulu visiwani na kueleza wanafunzi hao mbali na kunufaika kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini pia wananufaika kupitia udhamini wa Samia Suluhu Hassan ambao unatoa udhamini wa masomo ya elimu ya juu wa asilimia mia moja kwa wanafunzi wote wanaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.
Prof.Mkenda amesema Zanzibar ilitoa skuli 10 kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi na kunufaika na udhamini huo ikiwemo Skuli ya Sekondari ya Lumumba.
Aidha, Waziri Lela amesema mradi huo utaisaidia wizara, idara na taassisi zake kupata taarifa wanazozihitaji kitaaluma kwa usahihi na wakati bila ya kutumia mtandao na kueleza kwamba mradi huo upo chini ya Idara ya Tehama kutoka Wizara ya Elimu, Zanzibar inashirikiana na Serikali ya Ausralia ambao pia utahusisha ofisi zote za elimu za mikoa,wilaya na vituo vya elimu.
Kwa upande wa Pemba jumla ya wanafunzi 288 walipata daraja la kwanza kati ya hao137 kidato cha nne na 151 kidato cha sita.