NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, jamii ina wajibu mkubwa wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyabainisha hayo leo Januari Mosi, 2023 katika Uwanja wa Michezo wa Gombani ya Kale uliopo Chake Chake kisiwani Pemba katika shamrashamra za kutimiza miaka 59 ya Mapinduzi Matufuku ya Zanzibar.
Amesema, mazoezi ni muhimu ili kuondokana na maradhi mbalimbali, hivyo ni fursa nzuri kutenga muda angalau siku tatu kwa wiki ili kuuchangamsha mwili kupitia mazoezi.
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amevitaka vilabu vya michezo kuendelea kuimarisha umoja, upendo na mshikamano ili kutimiza dhamira ya Serikali kuimarisha michezo.
Vile vile, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali inatambua umuhimu wa michezo ya viungo na ndio maana ikaweka mkazo kuimarisha miundombinu ya michezo.
Awali, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliushukuru uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Jumuiya ya Vilabu vya Michezo Zanzibar (ZABESA) kwa kufanikisha tamasha hilo Kitaifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Tabia Maulidi Mwita amesema, kuwepo kwa sera ya michezo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na 2025.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiongoza matembezi wakati wa Tamasha la Bonanza la michezo yaliyowajumuisha viongozi mbalimbali na vikundi vya mazoezi kuanzia Tibirinzi mpaka Uwanja wa Gombani ya Kale katika maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Naye Mwenyeiti wa Jumuiya ya Vilabu vya Michezo (ZABESA), Bw.Said Suleiman amesema, jumuiya hiyo inaendelea na utaratibu wake wa kusafisha mazingira maeneo mbalimbali licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.