NA DIRAMAKINI
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaahidi vijana kushirikiana nao katika kufanya kazi za ujenzi wa maendeleo ya nchi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Kiongozi wa Matembezi ya Vijana wa (UVCCM), Lulu Saleh picha ya Rais wa Kwanza wa Zanziba,Hayati Abeid Amani Karume, wakati wa uzinduzi wa Matembezi ya Vijana wa (UVCCM) yaliyozinduliwa Januari 5,2023 katika viwanja vya Mapinduzi Square Michezani Muembe Kisonge Wilaya ya Mjini Unguja.(Picha na Ikulu).
Amesema, vijana ni nguzo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa taifa ndio sababu ya Serikali za SMZ na SMT zimeteua vijana wengi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwapatia uzoefu wa kuongoza nchi yao kwa uwezo na weledi wa kuchapa kazi na kuijenga nchi kiuchumi na maendeleo.
Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, vijana wana nafasi kubwa ya kutumikia taifa lao na kuliletea maendeleo sambamba na kuwaasa vijana hao kwamba wanapaswa kujitambua kwa kujiweka imara ili kufanikisha malengo ya ukombozi wa kweli kwenye jamii zao.
Aidha, amewaeleza kwamba kazi iliyo mbele yao ni kujenga nchi baada ya kupata uhuru pamoja na kuwakumbusha kwenye suala muhimu la kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamamo katika jamii ambayo ndio chachu ya maendeleo ya nchi ilipofikia.
Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwashauri vijana hao kushikamana na kusaidiana katika kutafuta na kujitengenezea ajira ili kujitatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kujitafutia maendeleo.
Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote ya vijana kwa lengo la kuwapatia fursa za ajira vijana kwa namna yoyote iliyo bora na sahihi kwa mijibu wa sheria na taratibu za nchi.

Pia amesema, serikali zote mbili za SMZ na SMT zimeweka mifumo mizuri ya kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia sekta za umma na binafsi, mifumo aliyoieleza kwamba imewaepusha vijana kuepukana na mambo maovu, kuwajenga vijana kuwa wazalendo raia wema kwa taifa lao na kuwafanya vijana kujiona fahari kufanya kazi za kujitolea katika kujiletea maeneleo ya nchi yao.
Dkt.Mwinyi amewataka vijana kutumia mbinu tofauti kwa kuwafundisha vijana wenzao jinsi ya kuwa wazalendo kwa kujiepusha kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo matumizi ya dawa za kulenya, udhalilishaji na vitendo vyote vya uvunjifu wa sheria za nchi.
Akizungmza kwenye hafla hiyo, Mlezi wa Umoja wa Vijana wa CCM, Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amewaasa vijana hayo kuzidisha nidhamu kwenye kutumikia chama chao na kuwaomba kuendelea kuisemea vizuri serikali yao na juhudi za maendeleo zinazofanywa na chama chao.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Abdalla Juma Mabodi amewaasa vijana hao kuhubiri maridhiano ya nchi ili kudumisha jamii yenye umoja na mshikamano katika kujenga taifa lenye maendeleo ya amani na utulivu.
Amesema, Chama Cha Mapinduzi daima kinaungamkono juhudi za serikali na lazima kifuate maagizo na maono ya viongozi wa nchi.