Rais Dkt.Mwinyi:Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika elimu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Zanzibar imedhamiria kuleta mapinduzi makubwa ya Sekta ya Elimu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe.Lela Muhamed Mussa kwa pamoja wakifungua pazia kuashiria ufunguzi wa Skuli mpya ya Sekondari ya Salum Tuky kwa-Binti Amran,viongozi wengine wakishuhudia katika sherehe za shamra shamra za maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,iliyojengwa na Serikali ya Mapinduzi kwa fedha Uviko-19 kupitia Shirika la Fedha Duniani (IMF). (Picha na Ikulu).

Ni kwa kuboresha miundombinu ya majengo ya kisasa na huduma zenye ubora ili kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Januari 6, 2023 kwenye sherehe za ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Salim Turky iliyopo Mpendae kwa bint Hamrani ikiwa ni mwendelezo wa kusheherekea miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema ,Zanzibar kwa sasa inastahili kuwa na skuli zenye ubora wa hali ya juu ili kuendana sambamba na hadhi ya Mapinduzi visiwani.
Amesema, mabadiliko ya elimu Zanzibar yatafikiwa kwa kuwa na ujenzi imara wa miundominu ya majengo ya kisasa yatakayochukua wanafunzi wachache kwenye madarasa, vifaa vya kisasa na mazingira mazuri ya kufundisha na kujifunza.

Aliongeza skuli ya Salim Turky ni mfano hai wa skuli zote anazotaka kuzijenga Zanzibar hadi kufikia Januari, 2025 pamoja na kukamilisha miradi mingine mikubwa ya maendeleo ili kuendana sambamba na hadhi ya miaka ya Mapinduzi iliyofikiwa kwa visiwa vya Unguja na Pemba.

“Skuli hii ndio mfano wa skuli zetu za ninazotaka ziwe nchini, skuli za ghorofa ambazo ndani yake kuna maabara ya sayansi, maktaba, vyumba vya kompyuta na madarasa wanafunzi wetu wasiozidi 45,”alielekeza Dkt.Mwinyi.
Alisema, serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha Zanzibar inapata madarasa ya kutosha, nyenzo bora za kusomea ikiwemo vitabu na walimu wenye sifa kulingana na fani zao ikiwemo kuongeza ajira za walimu wa sayansi na hesabati ili kuondosha kabisa changamoto ya uhaba wa walimu wa aina hiyo pamoja na kufanikisha skuli kuwa na mkondo mmoja badala ya miwili au mitatu kama awali.

Aidha, alieleza hadhi ya skuli zote za Zanzibar kwa sasa zinatakiwa kuwa na majengo ya ghorofa yaliyokamilika kwa huduma za kisasa na kuahidi kwamba ifikapo miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar anatarajia kufungua miradi mikubwa zaidi ya maendeleo.

Aidha, aliwataka watendaji wa Wizara ya Elimu kuhakikisha skuli inatoa huduma zinazoendana na hadhi yake kwa kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi.
Naye, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla alisema maendeleo mazuri ya elimu yanafikiwa kwa kuwa na miundominu imara ikiwemo vifaa vya kusomeshea, mazingira mazuri kama majengo ya kisasa na wachapa kazi ambao ni walimu wenye uweledi na uthubutu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa alisema ujenzi wa skuli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025 ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliahidi kujenga miradi malimbali ya maendeleo ikiwemo maradasa 1500 na sasa wamekamilisha ujenzi wa madarasa 1,200.

Alisema, Wizara ya Elimu imepiga hatua kubwa katika kukamilisha miradi yote iliyopanga na kwamba imeakisi dhima ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Khamis Said alisema ujenzi wa skuli hiyo umegharimu shilingi milioni 421.1ambao umejumuisha Maktaba, Maabara, chumba cha kompyuta, ofisi ya mwalimu mkuu, ofisi ya msaidizi mwalimu mkuu, ofisi tatu za walimu, chumba cha kusalia,vyoo 25,viti na meza 1305 kwa ajili ya wanafunzi wote.

Aliongeza Skuli ya Sekondari Salim Turky itaondosha msongamano kwenye skuli za Mwanakwerekwe na skuli jirani kwa wanafunzi wengi kusoma hapo.
Skuli ya Sekondari ya Salim Turky ni moja kati ya skuli mpya 45 zilizojengwa na Serikali ya Awamu ya Nane kwa fedha za ahuweni ya Uviko-19 Zanzibar,ambapo Unguja zimejengwa 23 na Pemba 22.

Aidha, skuli hiyo imepewa jina la Mbunge wa zamani wa jimbo la Mpendae,marehemu Salim Turky ili kuenzi mchango mkubwa wa maendeleo alioutoa Mbunge huyo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakati wa uhai wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news