NA MWALIMU MEIJO LAIZER
MARIDHIANO ni hatua inayofikiwa kwa dhana ya kuleta makubaliano ya pamoja, kwa jambo lenye masilahi kwa makundi mawili au zaidi yenye mtazamo au itikadi tofauti katika nchi husika.
Inapotokea makundi haya hayakubaliani katika mazingira na baadhi ya mambo, basi kwa taifa lenye wastaarabu wanakubalina kukutana meza moja kuzungumza namna ya kwenda ili kujikwamua katika hali ya kutoelewana na mambo haya huwa ni muhimu sana kufanyika wakati wa amani.
Aidha, inapobainika kama kuna jambo la namna hiyo kwa pande zote au upande mmoja basi kundi moja huleta hoja ya maridhiano kwa lengo la kutimiza Malengo Mahususi yaliyotarajiwa kwa makundi yote mawili na kuona kuna umuhimu wa kukaa pamoja ili kuzungumza.
Mathalani,mwaka 2007 nchi ya Kenya ilipitia katika wakati mgumu sana katika mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu, jambo ambalo lilifanya kuzaliwa kwa maridhiano ya kitaifa kwa kuyakutanisha makundi yote kinzani.
Maridhiano hayo yakawa ni baada ya kutokea mauaji ya baadhi ya watu na kufanya nchi hiyo kupoteza nguvu kazi ya taifa kutokana na zoezi zima la uchaguzi mkuu huo kutawaliwa na sintofahamu na kufanya uwepo wa vurugu na kusababisha viongozi wa kitaifa kupelekwa katika mahakama za kimataifa, kwa lengo la utetezi wa haki za binadamu.
Nchini kwetu Tanzania, suala la maridhiano limejitokeza katika vipindi mbalmbali vilivyopita na mpaka sasa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kujenga msingi uliyojengwa na waasisi wa Taifa letu.
Sote tunajua Uundwaaji wa Serikali ya Umoja wa kitaifa katika Serikali ya Zanzibar ni matokeo ya maridhiano hayo ambayo yalitokana na mnyukano wa kisiasa kati ya chama tawala na vyama vya upinzani, wakati huo chama chenye nguvu Tanzania Zanzibar kikiwa ni chama cha wananchi CUF.
Ni dhahiri maridhiano yana nguvu kubwa duniani, kwani ukitazama kwa mawanda mapana kwa sasa namna siasa za Zanzibar zinavyoleta na kuliweka taifa hilo pamoja, kujenga mshikamano,upendo na umoja wa kitaifa kwa Wazanzibar inafanya nchi hiyo kuwa na utulivu mkubwa na kufanya upatikanaji wa maendeleo ya haraka katika nchi.
Maamuzi ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kufanya maridhiano ya kitaifa na kudumisha uwepo wa demokrasia inabainisha mambo ya msingi yafuatayo;
Mosi,Uzalendo wa kiongozi Mkuu wa nchi, unafanya uwepo wa maridhiano jambo ambalo linaongozwa na dhamira njema kwa kiongozi huyo, kongole Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.
Pili,nidhahiri kuwa utashi wa kisiasa wa kiongozi mkuu wa nchi huchochea uwepo wa maridhiano katika Taifa husika jambo ambalo huleta umoja wa kitaifa na katika hili kongole Mheshimiwa Rais wetu, kwani umeonnesha upendo mkubwa kwa Taifa lako.
Tatu, maridhiano na demokrasia ni matokeo ya uimara wa uongozi wa chama kinachotawala Taifa letu (CCM), kwani umethibitisha ukongwe wake, kwa kuridhia kujengwa maridhiano ya kitaifa na kudumisha demokrasia ya kweli.
Ni dhahiri sote tunajua katika Bara la Afrika vipo vyama vya siasa vimefanya kazi kubwa ya harakati za uhuru na ukombozi katika nchi zetu za Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini leo vimepotea, yote haya ni udhaifu mkubwa wa kukosa uimara katika kujenga maridhiano katika nchi zao, kongole Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Chama Tawala kwa hatua hii kubwa ya kujenga Taifa letu katika msingi mzuri wa kidemokrasia na maridhiano kwa masilahi mapana ya Taifa letu.
Sote ni mashuhuda kwa nchi zilizokosa fursa ya maridhiano ya kitaifa. Tazama KANU nchini Kenya na nchi nyinginezo, tazama nchi ya Libya ambayo pia ilikumbwa na athari ya kukosekana kwa uimara wa chama tawala hadi sasa taifa hili lipo kwenye mateso makubwa ya janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Sote tunakubaliana kuwa, uimarishaji wa demokrasia na maridhiano katika Taifa lolote inaleta matokeo chanya katika maendeleo, uimarishaji wa uchumi wake wa ndani, kujenga twasira nzuri ya Taifa katika anga za kimataifa jambo hili huleta na kuimarisha diplomasia za kimataifa pia.
Kongole Mheshimiwa Rais wetu kwa hatua ya maridhiano ya kitaifa na kudumisha demokrasia kwa watu wako.
Mambo ya msingi ya kuzingatiwa na vyama vya siasa hasa vyama vya upinzani ikiwemo chama kikuu cha upinzani nchini CHADEMA.
Mosi,ni vema,vyama vyote vya siasa kuunga na kukubaliana na jitihada na dhamira njema ya Rais Dkt.Samia ya kuanzishwa kwa maridhiano na uwepo wa demokrasia kama taifa, kwani kwa kufanya hivyo nchi itaimarika zaidi na kutunza utaifa wake.
Pili,vyama vya siasa vibebe uzalendo mkubwa kwa Taifa letu na kuachana na masilahi binafsi ya vyama vyao ili Rais wetu aweze kutimiza ndoto yake ya kujenga nchi yenye maendeleo imara zaidi.
Tatu,vyama vya siasa vinawajibika kutunza amani yetu kwa kila kimojawapo kuheshimu dhamira njema ya Rais wetu ya kuleta maridhiano katika nchi, kwani kwa kufanya hivyo itakua na tija kwa maendeleo ya taifa letu.
Nne,maridhiano na demokrasia iweze kuwa dira ya kujenga umoja na mshikamano wetu kama Taifa, kadhalika ndani na nje ya vyama vyetu vya siasa.
Tano,uwepo wa maridhiano na kudumisha demokrasia katika nchi utasaidia taifa kupanga na kufikia malengo yake mahususi ya kuleta maendeleo kwa watu wake hasa katika nyanja mbalimbali kama vile masuala ya kiuchumi na shughuli zingine za kijamii.
Ni dhahiri kuwa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ameamua kujenga Taifa imara lenye upendo, mshikamano,umoja,amani na utulivu kwa watu wake.Sote, tuna kila sababu ya kukubali kwa dhamira njema maridhiano na kudumisha demokrasia kwa afya ya Taifa letu, tuipende nchi yetu kuliko tofauti za vyama vyetu vya siasa kwani nchi ni zaidi ya vyama.
Dhamira njema ya Rais wetu ni kuleta siasa safi na yenye tija kwa maendeleo ya nchi, hivyo Watanzania wote tuna kila sababu ya kukubali maridhiano na demokrasia ya kweli ili tuweze kufanya maendeleo endelevu kwa pamoja.
Uimara wa vyama Vya upinzani ni uimara wa chama tawala katika nchi yeyote, na udhaifu wa vyama vya upinzani kwa Taifa lolote ni udhaifu wa chama tawala katika Taifa..
Kongole Mheshimiwa Rais wetu kwa uzalendo na maamuzi makubwa uliyofikia kwa kudumisha demokrasia ya kweli na kufanya nchi yetu kujengwa katika Falsafa ya Maridhiano.
Sote kama Taifa tuna wajibu mkubwa wa kuungana na Rais wetu katika kujenga Taifa lenye Umoja na Mshikamano, kujenga Taifa lenye Upendo na Uzalendo wa kweli kwa kila mmoja wetu, kujenga Taifa lenye nguvu katika maendeleo yake na si vinginevyo, na kujenga Taifa lenye Amani na Utulivu kwa Watu Wake Wote.
Mwalimu Meijo Laizer
MNEC Mstaafu Wilaya ya Siha
0755898037
Tags
Habari
Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita
Makala
Maridhiano ya Kitaifa
Serikali ya Awamu ya Sita