Rais Dkt.Samia:Vyama vya Siasa Ruksa kufanya mikutano ya hadhara

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ametangaza maamuzi ya Serikali kuondoa zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) , Mhe. George Simbachawene, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Francis Mutungi, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Mohammed Ally Ahmed pamoja na viongozi wa Vyama Vya Siasa mara baada ya kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Januari 3, 2023.(Picha na Ikulu).

Aidha, Rais Dkt. Samia amevitaka vyama vya siasa kuikosoa na kuishauri Serikali kupitia mikutano ya hadhara kistaarabu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo.

Rais Dkt. Samia ametangaza maamuzi hayo leo wakati akizungumza na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa 19 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Samia amesema Serikali imedhamiria kuukwamua mchakato wa kupata Katiba mpya baada ya kukaa na kukubaliana na vyama vya siasa.

Vile vile, Rais Dkt. Samia amesema, hatua hiyo itazingatia hali halisi ya nchi, uwezo wa kiuchumi pamoja na mila na desturi zetu.

Wakati huo huo, Rais Dkt.Samia amesema Serikali inajiandaa kurekebisha Sheria anuai zikiwemo Sheria za Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa ili kujenga taifa lenye umoja.

Rais Dkt.Samia amesema, ili taifa liwe moja lazima kuwe na maridhiano baina ya vyama vya siasa kwa lengo la kuendesha taifa lenye amani na utulivu kwa maendeleo ya taifa letu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news