Salamu za Mwaka Mpya: NABADILISHA FIKRA

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Januari Mosi, 2023 ni siku ya kwanza kabisa ya safari ya kuziendea zaidi ya siku 360 za mwaka huu mpya. Ni safari ambayo inaanza huku kila mmoja wetu akiwa tayari ana mipango yake, ambayo anaamini kwa uweza wa Mungu ndani ya mwaka huu itakwenda kutimia.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema, ameamua kubadilisha fikra ili afanye kazi ambazo zitastawisha maendeleo yake, jamii na Taifa kwa ujumla, Je? Wewe umeamua kubadilisha fikra. Endelea;

1.Nabadilisha fikra,
Ili niwe mtu bora,
Niyaache ya kukera,
Nifanye maendeleo.

2.Nafungua ukurasa,
Nikiwa nayo hamasa,
Ya hovyo sitayagusa,
Nifanye maendeleo.

3.Ninaanza mambo mapya,
Hata kama yaogofya,
Hayo kwangu ndiyo afya,
Nifanye maendeleo.

4.Sasa zatosha safari,
Zisizoleta uturi,
Siitaki tena hari,
Nifanye maendeleo.

5.Marafiki wadowezi,
Na sera za kichochezi,
Kwangu hawapati kazi,
Nifanye maendeleo.

6.Sasa nasafisha njia,
Kwa kweli nimepania,
Malengo kuyafikia,
Nifanye maendeleo.

7.Kunizoeazoea,
Kunichekeachekea,
Sasa ninapotezea,
Nifanye maendeleo.

8.Shamba ninapanda ngano,
Kesho nipate mavuno,
Vingine nasaga meno,
Nifanye maendeleo.

9.Nabadilisha fikra,
Sitaki tena hasara,
Wala mambo ya kukera,
Nifanye maendeleo.

10.Mambo ya kwenda kusini,
Au ya kaskazini,
Cha maana sikioni,
Yapinga maendeleo.

11.Yale nitakayofanya,
Ninataka kukusanya,
Wala siyo kutapanya,
Nifanye maendeleo.

12.Naamini Mungu yupo,
Hata maamuzi yapo,
Na utashi wangu upo,
Nifanye maendeleo.

13.Mwaka huu wa Baraka,
Si wa virakaviraka,
Taniwezesha Rabuka,
Nifanye maendeleo.

14.Mimi ninaanza leo,
Utaona matokeo,
Kazi si upendeleo,
Nifanye maendeleo.

15.Hivi ninajiapisha,
Bidii ninazidisha,
Ni moto ninauwasha,
Nifanye maendeleo.

16.Mungu amenifikisha,
Kweli kanifurahisha,
Sasa ninaliamsha,
Nifanye maendeleo.

17.Kama ni rafiki yangu,
Upendaye mambo yangu,
Jali msimamo wangu,
Nafanya maendeleo.

18.Ya kale yameshapita,
Kichwani nimeyafuta,
Nimeshapakwa mafuta,
Nifanye maendeleo.

19.Sitabaki vilevile,
Kwenda mwendo uleule,
Kama niko mwaka ule,
Nafanya maendeleo.

20.Kama nimechanja chale,
Kufanya nisonge mbele,
Kurudi nyuma ukale,
Nafanya maendeleo.

21.Ninaandika kwa wino,
Herufi kubwa maneno,
Nimejizatiti mno,
Nifanye maendeleo.

22.Mungu wangu wa mbinguni,
Uwe nami maishani,
Nisibaki barazani,
Nifanye maendeleo.

23.Yale ya kuchelewesha,
Kila siku kunichosha,
Hayawezi nikalisha,
Nafanya maendeleo.

24.Kile kinawezekana,
Hicho kitawezekana,
Kushindwa ninakukana,
Nifanye maendeleo.

25.Sasa Niko mwaka mpya,
Nitafanya mambo mapya,
Yale kwangu ni ya afya,
Nifanye maendeleo.
(Yeremia 29:11)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
Iwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news