Sekta ya Afya imeboreshwa zaidi-Makamu wa Rais

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Philip Isdori Mpango amesema,Sekta ya Afya imeboreshwa zaidi nchini ili iweze kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi.
Mtambo wa Uchunguzi wa matatizo ya Moyo hospitali ya Benjamin Mkapa.

Hayo yamesemwa leo Januari 20, 2023 kupitia hotuba ya Makamu wa Rais iliyosomwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.Angellah Kairuki (Mb) katika hafla ya kuufahamisha umma mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Dodoma.

"Katika eneo la afya. Leo Watanzania wamepata fursa ya kufahamu kuwa Serikali yao imeboresha kwa kiwango kikubwa huduma za afya. Mtanzania unayeishi Dodoma huna haja tena ya kwenda Dar es Salaam au nje ya nchi kupata huduma za kibingwa bobezi kama vile upandikizaji wa figo, matibabu ya moyo, vipandikizi kwenye magoti na nyonga (Hip and total Knee Replacement), matibabu ya ubongo na mishipa ya fahamu (upasuaji wa mishipa ya fahamu, upasuaji wa ubongo na upasuaji uti wa mgongo).

"Matibabu haya yanapatikana katika Hospitali yetu ya Kanda ya Benjamin Mkapa. Hili limetokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya kisasa, vifaa tiba na wataalam bobezi wa fani mbalimbali za afya.
Moja wapo ya chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

"Kwa hili, Dodoma imepata fursa kubwa ya kufanya utalii wa kimatibabu (medical tourism) kwa wagonjwa wanaotoka mikoa ya jirani na hata nchi za jirani,"amefafanua Waziri Kairuki kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt.Mpango.

Pia amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za Watanzania. Amesema, Serikali imewekeza fedha nyingi kujenga miundombinu ya afya, na kusomesha na kuandaa wataam na wahudumu wa afya.

"Nitumie fursa hii kuwataka watumishi wote wa afya nchini kutoa huduma bora ya kujali mtanzania kama Serikali ilivyokusudia,"amesema.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais amewapongezz viongozi wote wanaoongoza taasisi mbalimbali za umma, binafsi, dini na vyama vya siasa Dodoma kwa mshikamano na ushirikiano mkubwa ambao unaleta tija kwa maendeleo ya Mkoa wa Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news