NA JOHN MAPEPELE
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa ndugu Fadhili Rajabu Maganya amepongeza jitihada za Serikali na Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa za kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo huku akiwataka wataalam kusimamia na kutekeleza miradi kwa wakati ili kupata matokeo tarajiwa.

Pamoja na wadau wengine, ndugu Maganya amemtunikia Mhe. Mchengerwa hati ya shukrani kwa kutambua mchango wake mkubwa anaoutoa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo la Rufiji.
Aidha, ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuonyesha mshikamano na ushirikiano kwenye jumuiya zote za chama katika kuwatumikia wananchi huku akiitaka mikoa yote kuiga mfano huo.
Amewataka watendaji wa Chama Cha Mapinduzi katika ngazi zote nchini kuwa na nidhamu katika kusimamia fedha zote za miradi zinazotolewa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi huku akisisitiza kuwa wao ndiyo jicho la chama katika ngazi husika.

“Ninawapa makali ya kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini jambo la kwanza ni kusimamia kero,” amesisitiza Mwenyekiti Maganya.
Mbali na hayo, amewahimiza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kukisemea chama hicho mambo makubwa ya kimaendeleo ambayo yamefanyika katika kipindi hiki kifupi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.