NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema uamuzi wa Serikali utakaofikiwa baada ya mashauriano ya kina yanayoendelea juu ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote utazingatia maslahi ya wananchi wote na hasa wenye kipato kidogo kwa lengo la kumwezesha kila mwananchi kupata huduma bora za afya na kwa gharama nafuu.

Aidha amesema Serikali inaendelea kupokea maoni na ushauri wa watu mbalimbali kuhusu kuanzishwa kwa mfuko huo.

Amesema hajaridhishwa na taarifa ya Mkoa kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri za Shinyanga.

Vilevile amemtaka Mthamini Mkuu wa Serikali kukamilisha uhakiki na uthamini wa mali na mashamba ya wananchi wa mwadui walioathirika na bwawa la taka sumu kupasuka na kuwalipa haki zao haraka iwezekanavyo.
Akiwa katika eneo la Kagongwa,Makamu wa Rais ameagiza kutafutwa na kuchukuliwa hatua mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Athuman Yusuph kwa kumtelekeza mwanamke anayefahamika kwa jina la Prisca Nyanda ambaye ni mlemavu akiwa na watoto wawili na hivyo kulazimika kutembea na watoto hao katika baiskeli yake wakati wote akitafuta riziki na mahitaji ya watoto hao.
Makamu wa Rais ametoa shilingi milioni tano wakati akiwaongoza wananchi na viongozi wa eneo hilo katika kumchangia mama huyo fedha zitakazomwezesha kujikimu na kufanya biashara.

Zaidi ya shilingi milioni sita na laki nane zimepatikana katika harambee hiyo pamoja na vyakula mbalimbali ikiwemo unga na mchele.