Serikali yaja na mipango kabambe shule za kata nchini

NA OR TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayesimamia Elimu, Dkt.Charles Msonde amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Serikali kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekodari (SEQUIP) inatarajia kujenga shule mpya za sekondari za kata 184 ambapo itajengwa shule moja kila halmashauri.

Dkt. Msonde ameeleza hayo Januari 6,2023 katika ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika Halmashauri ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati akikagua Shule Maalum ya Wasichana ya iitwayo Dkt.Samia Suluhu Hassan.

“Kupitia Mradi wa Kuboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) katika mwaka wa fedha 2021/22 tayari zimejengwa shule 232 za kata na katika mwaka huu wa fedha kabla ya kufika mwezi Juni, zitajengwa shule mpya 184 za kata, moja kiła halmashauri,” amesema Dkt.Msonde.

Dkt.Msonde ameeleza kuwa, ujenzi wa shule za kata utaenda sambamba na ujenzi wa shule mpya tano nyingine za wasichana za mikoa ili kuongezea kwenye shule 10 ambazo ujenzi wake kwa awamu ya kwanza upo katika hatua za ukamilishaji kwa gharama ya silingi bilioni 30.

Aidha,Dkt.Msonde amefafanua kuwa, ujenzi wa shule hizo za kata utagharimu shilingi milioni 600 na utakuwa na awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itatolewa shilingi milioni 470 kujenga miundombinu yote ya shule na shilingi milioni 130 itatolewa katika awamu ya pili kujenga nyumba za walimu na kununua vifaa via TEHAMA vya wanafunzi kujifunzia.

Wakati huo huo, amewatoa hofu wazazi kwa kueleza kuwa Serikali imeweka jitihada kubwa ya kuboresha shule zote za kata kwa kuboresha miundombinu ili kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya sekondari kwa kujenga shule ya sekondari kila kata.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news