NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Tanzania imepokea msaada wa vifaa vya kujikinga na magonjwa ya milipuko kwa ajili ya watumishi wanaotoa huduma za afya na wateja wanaowahudumia,kutoka serikali ya Uingereza.
Makabidhiano ya vifaa hivyo yamefanyika Bohari ya Dawa (MSD) Keko Dar es Salaam,ambapo Mganga Mkuu wa serikali Prof. Tumaini Nagu amepokea vifaa hivyo kwa niaba ya serikali kutoka kwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, Kemi Williams.
Akipokea msaada huo Prof. Nagu ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa vifaa hivyo na kueleza kuwa vifaa vya kujikinga na magonjwa ya mlipuko ni muhimu ili kupunguza hatari ya watoa huduma kuambukizwa wanapotekeleza majukumu yao. Vifaa hivyo vitasambazwa na MSD kama wizara ilivyoelekeza.