Serikali yawataka wakuu wa mikoa, wilaya kuwa walezi wa jumuiya za wafanyabiashara

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ametoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini kuhakikisha wanakuwa walezi wa jumuiya za wafanyabiashara na kuwa nao karibu katika kila jambo wanalotaka kulifanya ili watoe ushauru wenye tija katika kujenga na kustawisha biashara hapa nchini.
Aidha, amewashauri Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri, Mameya wote nchini kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania kutengeneza mfumo mzuri utakaomfanya kila mfanyabiashara anapotaka leseni ya biashara aipate kwa haraka bila usumbufu.

Kigahe ameyasema hayo Januari 27, 2023 alipokuwa akihutubia Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Iringa kwa lengo la kujadiliana na kushauriana kuhusu masuala muhimu ya maendeleo ya biashara na changamoto zake katika mkoa huo.
Kigahe pia amewasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote nchini waitishe mikutano ya majadiliano mara kwa mara kati ya Serikali na Sekta Binafsi kupitia Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya ambayo yapo kisheria kwa lengo la kutatua kero za Wafanyabiashara na Wawekezaji kwa wakati kwa kuwa ndio injini ya uchumi wa taifa.

Kigahe pia ametoa rai kwa Watumishi wote wa Taasisi za Umma zinazohusika na utoaji wa leseni na vibali mbalimbali kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na wakati wote kuhakikisha utoaji wa huduma hizo unalenga kuwezesha na siyo kukwamisha biashara.
Akijibu maoni na hoja zilizotolewa, Kigahe amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara za kisekta pamoja na Serikali za Mitaa itahakikisha inatatua changamoto zote zilizowasilishwa zinatatuliwa haraka iwezekanavyo ikiwemo suala la sehemu ya machinga, pamoja na mgogoro wa Bajaji na Daladala mkoani humo.

Vilevile, amesema endapo bidhaa nyingi zinazozalishwa katika Mkoa huo hususani zile za mazao ya Misitu, Mazao ya kilimo na mifugo ikiwemo mahindi, mchele, mbogamboga na matunda zikichakatwa na kuhifadhiwa katika viwango vinavyokubalika kimataifa vitawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kunufaika na fursa ya masoko ya baina ya nchi, kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeingia mikataba kama EAC, SADC, AfCFTA na AGOA.
Aidha, Amesema Wizara itaendelea kutekeleza ipasavyo Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) ili kuendana na kasi ya Serikali ya kukuza na kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Viwanda na Biashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news