Shah aonesha dhamira kufungua kiwanda cha kuzalisha na kusambaza dawa za binadamu Tanzania

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mtendaji wa KingJada Hotels & Apartments Ltd ambaye ni Mkurugenzi wa Swastik Trading Ltd yenye makazi yake jijini Mwanza, Congo, Dubai na India akiwa pia ni mmiliki wa Pharmacy Retail Chain, Sanjay Madanraj Shah anatarajia kufungua kiwanda cha uzalishaji na usambazaji wa dawa za binadamu nchini.

Hayo yamesemwa Januari 27, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano KingJada Hotels & Apartments Ltd, Morocco Square jijini Dar es Salaam,Risasi Mwaulanga wakati uongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na KingJada Hotels and Apartment Ltd wakisaini mkataba wa kihistoria.

Ni kwa ajili ya upangishwaji na uwekezaji wa ubia kwa ajili ya huduma ya hoteli katika Mradi wa NHC Morocco Square jijini Dar es Salaam.

Amesema,Shah mwenye uzoefu mkubwa kutoka nchini India kutokana na uendeshaji wa biashara mbalimbali ikiwemo hoteli ameamua kuelekeza uwekezaji mkubwa nchini kutokana na dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa wawekezaji. KingJada Hotels and Apartment Ltd ni ubia wa kwanza nchini Tanzania na barani Afrika.

"Bw.Sanyaj Madanraj Shash ni Mkurugenzi wa Swastik Trading Ltd yenye makazi yake Mwanza, Congo, Dubai na India, pia ni mmiliki wa Pharmacy Retail Chain nchini India, pia anajipanga kufungua kiwanda cha uzalishaji na usambazaji wa dawa za binadamu hapa nchini Tanzania,"amefafanua Mwaulanga.

Amesema, wawekezaji wengi akiwemo Sanyaj Madanraj Shash wanavutiwa na aina ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"KingJada Hotels inajumuisha uwekezaji wa ubia na Mkurugenzi wa kizalendo aliyebobea katika uendelezaji wa huduma za hoteli kwa maana ya madam Nyangeta, lakini pia uongozi wa NHC na KingJada Hotels tunaamini tuna dhamira ya pamoja kuleta mageuzi ya kisekta kwa maana ya sekta ya utalii na sekta ya hoteli Tanzania.

"Mkurugenzi amesema hapa kutakuwa na watu wengi sana, watu watakuja hapa kupata huduma, kupiga picha na kadhalika,kwa hiyo tutakuwa na watu mbalimbali kwa sababu mazingira ya demokrasia na siasa za nchi yetu chini ya Rais Samia yapo vizuri sana.

"Rais Samia ameifungua nchi yetu, watu watakuja wengi na Tanzania imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya Afrika na Dunia tunatarajia kuwa na wageni wengi kupitia matokeo ya filamu ya Royal Tour na ndiyo iliyowavutia kuwekeza katika hoteli hii,"amefafanua.

"Ninapenda kupongeza kazi kubwa zilizofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye yeye na wateule wake katika sekta mbalimbali imetufanya wawekezaji kujenga imani kubwa katika suala zima la uwekezaji kwa kutujengea mazingira ya kiuwekezaji na kutoa fursa ya majadiliano.

"Narudia tena, Serikali imetoa mijadala mipana na ya uwazi jinsi gani tuendeshe uchumi wetu na jinsi gani tufanye uwekezaji usio na mashaka na jinsi gani wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza na kuamini kwamba Tanzania ni sehemu salama,"amesema.

Kupitia uwekezaji wa hoteli hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kutoa huduma siku za karibuni, Sanjay Madanraj Shah anatarajia kuwekeza zaidi ya dola milioni 60.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news