TRA yakusanya Trilioni 12.46/- nusu ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2022/2023

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2022/23 ambacho kinajumuisha mwezi Julai 2022 hadi Desemba 2022 imefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 12.46 ikiwa ni sawa na asilimia 99 ya lengo la makusanyo ya shilingi Trilioni 12.48.

Hayo yamebainishwa Januari Mosi, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Alphayo J.Kidata.

Amefafanua kuwa, makusanyo hayo ni ongezeko la shilingi Trilioni 1.35 ikilinganishwa na kiwango cha makusanyo cha Shilingi Trilioni 11. 11 kilichokusanywa kwa kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha 2021/22. "Ongezeko hili ni sawa na ukuaji wa makusanyo wa asilimia 12.2,"ameeleza.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, mamlaka hiyo katika kipindi cha mwezi Desemba 2022 ilifanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 2.77 kati ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 2.60.

"Makusanyo haya ya mwezi Desemba 2022 yana ufanisi wa asilimia 106.5 sawa na ukuaji wa asilimia 10.3 ukilinganisha na makusanyo ya mwezi Desemba mwaka 2021 ya shilingi Trilioni 2.51,"amebainisha.

Amefafanua kuwa, pamoja na makusanyo hayo kuvuka lengo la mwezi Desemba 2022, hicho kinakuwa ndicho kiwango cha juu zaidi kuwahi kukusanywa kwa mwezi tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996.

"Tunaendelea kuwashukuru walipakodi na wadau wetu mbalimbali kwa kujitoa kwenu katika kipindi cha nusu ya mwaka ambapo mwenendo wa ulipaji kodi kwa hiari na mahusiano baina ya mamlaka na walipakodi umeendelea kuimarika kwa kiwango cha kuridhisha.

"Kwa niaba ya Menejimenti ya TRA na kwa niaba yangu binafsi (Kamishna Mkuu wa TRA) napenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa kutuwezesha kufikia ufanisi huu wa asilimia 99,"amefafanua.

Wakati huo huo,mamlaka hiyo imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuisaidia katika utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kiutendaji.

Amesema, TRA imeendelea kufanyia kazi maelekezo na miongozo ya Serikali juu ya namna bora ya kukusanya mapato bila matumizi ya nguvu na hivyo kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.

"Serikali imeendelea kuisaidia mamlaka katika ujenzi na matumizi ya mifumo inayochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji kazi wetu. TRA itaendelea kuboresha huduma kwa walipakodi wetu kwa kuzingatia dhana ya uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kujenga taswira yenye kuaminika katika jamii,"amefafanua Kamishna Mkuu wa TRA, Bw.Kidata.

Aidha, amebainisha kwamba, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna umuhimu wa kuongeza kiwango cha makusanyo kwa kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari kwa walipakodi ili kuiwezesha Serikali kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa wananchi wote kama ulinzi, miundombinu ya barabara, huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji, umeme na nyinginezo.

"Hivyo basi, mamlaka inawakumbusha walipakodi na wadau wasiozingatia sheria, kanuni na taratibu za ulipaji kodi kubadilika ili kuepuka riba, adhabu, kesi na usumbufu unaoweza kuepukika,"amesisitiza Kamishana Mkuu wa TRA.

Mbali na hayo, Kamishna Mkuu wa TRA amebainisha mambo kadhaa wakati safari ya mwaka 2023 ikiwa imeanza.

"TRA inatoa rai na kusisitiza yafuatayo kwa wadau wetu wote, wauzaji wote wa bidhaa na huduma mbalimbali wahakikishe wanatoa risiti sahihi za kielektroniki yaani EFD katika kila mauzo wanayofanya.

"Wanunuzi wote wadai risiti sahihi za kielektroniki katika kila manunuzi ya bidha au huduma wanayopatiwa, kupitia kudai risiti sahihi ya bidhaa au huduma unayopatiwa unakuwa umetoa mchango mkubwa kwa Taifa letu.

"Walipakodi wanapaswa kuwasilisha ritani sahihi, kulipa kodi stahiki na kulipa madeni ya kodi kwa wakati.Wazalishaji na waingizaji wa bidhaa nchini zinazotozwa ushuru wa bidhaa wanapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya stempu za ushuru wa bidhaa.

"Pia walipakodi na wadau wetu waendelee kuhudhuria mafunzo mbalimbali yanayotolewa na mamlaka juu ya elimu ya kodi na matumizi ya mifumo ya usimamizi wa kodi ili kujijengea uwezo,"amefafanua kwa kina Kamishna Mkuu wa TRA.

Wakati huo huo, Bw.Kidata amesema, mwenendo wa ulipaji kodi na mahusiano mazuri baina ya mamlaka na walipakodi utaendelea kuimarika na hivyo kuwezesha kufikiwa lengo la makusanyo ya shilingi Trilioni 24.76 kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news