UVUMILIVU MARADUFU

NA ADELADIUS MAKWEGA

OKTOBA 6, 1996 Jimbo la Temeke mkoani Dar es Salaam lilifanya uchaguzi wa Ubunge uliomchagua marehemu Augustine Mrema kuwa Mbunge wa jimbo hilo huku CCM ikipoteza jimbo hilo mbele ya marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Julius Nyerere wakishuhudia hilo umbali mchache na makazi yao naye Rais Benjamin Mkapa akiwa miezi michache madarakani.

Siku chache kabla ya Jumapili ya Oktoba 6, 1996 mwanakwetu alitoka Shule ye Sekondari ya Kinondoni Muslim kuelekea eneo la Mtoni kwa Dosa kando ya Daraja la Treni juu Barabara chini-Mtoni Mtongani, Temeke Dar es Salaam kama ukiwa unakwenda Mbagala kushoto chini ya daraja hilo pana njia inaingia katika mji mdogo, ambapo kuna makazi ya watu wengi masikini. Hapa palikuwa na sehemu pana uwazi kiasi ndipo siku hiyo mkutano wa NCCR Mageuzi ulikuwa unafanyika.

Mwanakwetu alipofika hapo alikuta umati umejaa na huku viongozi wa NCCR wa Wilaya ya Temeke na wa Kitaifa walijaza eneo lililozibwa kwa turubai mbele ya umati mkubwa.

Viongozi kadhaa wa NCCR–Mageuzi wakubwa kwa wadogo walikuwapo kumnadi mgombea wa Ubunge wa chama chao marehemu Augustine Mrema, hapo walikuwa wanapokezana mmoja mmoja kuongea. Mwanakwetu anakumbuka majina kama Masumbuko Lamwai na Charles Nyerere (hawa walikuwa wabunge wa NCCR) na Mabere Marando waliokuwa wakiongea kwa kupokezana vizuri sana wakiyapanga mawazo yao mbele ya umati mkubwa mmoja baada ya mwingine.

Maelezo ya viongozi wa chama hicho waliokuwa na majina makubwa makubwa yalinukuliwa mno na vyombo vya habari lakini maelezo ya majina ambayo hayakuwa maarufu sana hayakunukuliwa na hayafahamiki kwa Watanzania wengi ambao hawakulishuhudia tukio hilo.

Miongoni majina ambayo hayakuwa maarufu sana ni Dkt. Hassani Chewapoma, alipoalikwa jukwaani atoe salaam kutoka NCCR Mageuzi Kilimanjaro kwa wapiga kura wa Jimbo la Temeke na pia amnadi mgombea wao mkutanoni hapo alisema mambo mengi.

Kumbukumbu za mwanakwetu hazielezi kama Dkt.Chewapoma alikuwa Dakitari wa Tiba au Daktari wa Falsafa, lakini kumbukumbu hizo zinaeleza kuwa daktari huyu alipoalikwa aliwasalimu watu wa Mtoni Mtongani huku alijitambulishwa cheo chake kuwa ni mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Kilimanjaro, aliendelea kusema kuwa yeye kwa imani yake ni Muisilamu na anajitahidi mno kuzishika nguzo za dini hii.

Mwenyekiti huyu wa NCCR wa mkoa huo akasema kuwa wana NCCR Mageuzi Kilimanjaro ambao wengi wao ni Wakristo walimchangua yeye (Hassani) Muisilamu kuwa mwenyekiti wao na kukiongoza chama hicho hadi kupata wabunge kadhaa katika uchaguzi wa mwaka 1995 mkoani humu.

Akaongeza kuwa uwepo wake katika mkutano huo anawaomba wapiga kuwa wa Jimbo la Temeke wamchague ndugu Augustine Lytatonga Mrema kuwa mbunge wa Temeke.

“Wapiga kura tambueni kuwa Temeke haichagui imamu, bali mnachagua mtu wa kuwasemea bungeni mambo yenu na ninaamini kuwa ndugu Augustine Mrema ataifanya kazi hii vizuri.”

Mwanakwetu akiwa amevali suruali ya rangi samawati yenye weusi na shati jeupe la mikonomirefu lililochomekewa vizuri, maridadi na mikononi mwake akiwa amebeba mkoba alimsikiliza vizuri Dkt Hassani Chewapoma na salaam zake kutoka NCCR Mageuzi Kilimanjaro.

“Watu wa Kilimanjaro wao wanachoangalia ni uwezo wa mtu katika nafasi anayoiomba na ndiyo maana niliwashinda Wakristo kadhaa katika uenyekiti wa NCCR Mageuzi mkoani Kilimanjaro.”

Kiongozi huyu kwa sasa mwanakwetu hana taarifa zake alipo na alipomaliza kuongea hayo aliwaomba wananchi wote waliokuwapo mkutanoni akiwamo mwanakwetu wafanye jambo moja kwa pamoja.

“Watu wote simameni, ishike CCM mikononi mwako, alafu iweke chini, alafu nyanyua mguu wako, CCM kanyaga, naombeni mjibu CCM kanyaga.”

Watu mkutanoni wakawa wanajibu CCM kanyaga. Mwanakwetu akamuuliza jirani yake sasa ni CCM kanyaga au CCM ndiyo ipo chini na miguu yetu inaikanyaga? Jirani wa mwanakwetu akasema kwa ukali “Wewe mfanyakazi wa benki acha mambo yako hapa sisi tunaikanyaga CCM tu.”

Baada ya zoezi hilo Dkt Hassani Chewapoma alimualika Augustine Mrema apande jukwani na akaongea kwa kirefu kwa matamshi yake ya kichaga aliomba kura na mkutano huo kuisha salama na hapo mwanakwetu akarudi nyumbani kwake Mbagala.

Oktoba 6, 1996 ilifika uchaguzi ulifanyika na mbao za matokeo zilionesha kuwa Augustine Mrema wa NCCR Mageuzi alipata kura 54,840 Abdul Cisco Mitiro wa CCM alipata kura 33,113, Hiza Tambwe CUF alipata kura 3324, Alec Che Mponda wa TPP kura 515 Mege Omari wa UMD kura 422, Samson Msambara CHADEMA alipata kura 217, Legile Msonde wa UPDP alipata kura 162, Ndembe Abdallah wa Pona alipata kura 120, Rashidi Mtuta wa NRA alipata kura 114 Brighton Nsanya wa NLD alipata kura 69 na Shaban Matembo wa UDP alipata kura 67.

Hilo ni tukio la miaka 27 iliyopita, mwanakwetu leo hii anakumbusha tukio hilo kwa hoja kuwa wana siasa wa Tanzania wanahitajika kuwa na uvumilivu mkubwa kwa pande zote mbili; vyama pinzani na chama tawala.

Chama tawala kinahitaji kuwa na uvumilivu mara dufu maana katika uchaguzi huo uliosimuliwa Rais Benjamin Mkapa alionesha umahiri mkubwa wa ustamilivu kwa maamuzi ya wapiga kura vinginevyo angeweza kufanya lolote lile kwa mamlaka yake.

Uvumilivu huo unahitajika hata kwa wapiga kura na wapenzi wa vyama vya siasa wakiwa katika mikutano vya vyama vingine kama kisa hiki kilivyosimuliwa.

Kwa heri
makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news